Jamii ya Kiislamu Nchini inapaswa
kufuata vilivyo mafundisho sahihi aliyokuwa akiyasimamia Kiongozi wa
Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad { SAW } ili Jamii hiyo ipate fursa
nzuri ya kuishi katika maisha ya furaha na ustaarabu wa maendeleo
makubwa ndani ya Dunia hii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla ya maulidi ya uzawa wa
Mtume Muhammad { SAW } yaliyoandaliwa na Chuo cha Samail Academy na
kufanyika katika Msikiti Rahman uliopo Gombani Mjini Chake chake
Kisiwani nPemba.
Balozi Seif alisema kigezo chema
alichokuwanacho Kiongozi huyo wa waislamu kilijikita zaidi katika
kusimamia vyema suala la kudumisha amani katika Dunia, kuleta umoja
baina ya waislamu, kujikubalisha kuishi na mayatima sambamba na watu
wa rika zote bila ya ubaguzi.
Aliupongeza Uongozi wa Chuo cha
Samail Academy kwa juhudi zao walizozichukuwa na hatua waliyoifikia
katika kuijenga jamii kitaaluma na maadili yanayokubalika.
Hata hivyo alionya kwamba wapo
baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia vibaya elimu waliyobarikiwa kwa
kupotosha wenzao wasiokuwa nayo ili kufikia malengo yao binafsi.
“ Kuna Watu huitumia elimu
kuwageuza wenzao kuwa ngazi ya kupandia kuyafikia malengo yao
binafsi. Mwenyezi muungu hayataki mambo hayo. Tutumie elimu kwa
kuelimisha wengine “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alisema mafanikio makubwa kitaaluma
na kijamii yatapatikana endapo jamii itajikubalisha kujituma katika
misingi ya uaminifu licha ya changamoto za kimaisha
zinazowazunguuka katika maeneo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
akiridhia kukubali kuwa mlezi wa chuo hicho cha Samael Academy
aliahidi kuzishughulikia changamoto zinazowakabili Walimu na
Wanafunzi hao kwa kutoa mchango wake kadri hali itakavyoruhusu.
Akisoma Risala Mudiri wa Samaeil
Academy Sheikh Said Abdulla Nassor alisema Taasisi hiyo iliyoasisiwa
mwaka 2012 na kusajiliwa rasmi Mwaka 2014 inajishughulisha na masuala
ya kijamii katika maeneo mbali mbali hapa nchini.
Mudir Said alisema Samael Academy
imejikita katika kusaidia jamii katika uchimbaji wa visima,
kuunganisha Madrasa kuwa na nguvu za pamoja kuwakusanya watoto yatima
kwa kuwajengea mazingira bora ya kielimu na maisha yao ya baadae
pamoja na kuanzisha mafunzo kwa walimu wanaotoa hotuba misikitini.
Alisema yao mafanikio makubwa tokea
kuanzishwa kwa taasisi hiyo akizitaja kuwa ni pamoja na kuzikusanya
na kuzisajili madrasa zipatazo 95 zenye wanafunzi elfu 10,995,
kusajili mayatima 712 pamoja na kuzitembelea madrasa kwa kuangalia
changamoto zinazozikabili.
Mudiri huyo wa Samael Academy Sheikh
Said Abdulla Nassor alifahamisha kwamba moja kati ya jambo lililopewa
kipaumbele na taasisi hiyo ni kuwaendeleza wanafunzi na vijana
waliofanikiwa kumaliza kuhifadhi juzuu 30 za Quran tukufu.
Ata hivyo Sheikh Said Abdulla Nassor
alielezea changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo akizitaja kuwa ni
pamoja na vikwazo kwa baadhi ya watendaji wa taasisi za umma
wanavyovitoa kwa Taasisi hiyo pamoja na usumbufu wa vifaa vya msaada
vinavyotolewa wanafadhili wakati wa kutolewa bandarini.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika
hafla hiyo ya Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } Afisa
mdhamini Wizara ya Katiba na Sheria Pemba Bwana Omar Khamis alisema
Samel Academy tayari imeshaonyesha nia sahihi ya kutaka kusaidia
jamii hapa nchini.
Sheikh Omar alisema Taasisi hiyo iko
mbioni kujenga misikiti mikubwa mitatu Kisiwani Pemba,maandalizi ya
ujenzi wa chuoKikuu cha Kiislamu Chamanangwe pamoja na ujenzi wa chuo
cha Amali Chake chake Pemba.
Alisema uanzishwaji wa chuo hicho
cha amali umelenga kuwajengea mazingira mazuri wanafunzi watakaopata
taaluma kwenye taasisi hiyo na maandalizi yameanza katika kuhakikisha
kwamba wanafunzo hao wanapata ajira ndani na nje ya Nchi.
Alifafanua kwamba Nchi za Saudi
Arabia na Iraq ambazo zimeamuwa kujitolea kusaidia harakati za ujenzi
wa chuo hicho cha amali Kisiwani Pemba zimekubali kuwapokea wanafunzi
wa chuo hicho kwa kuwapatia fursa za ajira katika Mataifa hayo.
Akitoa salamu zake Rais wa Samael
Academy Sheikh Nassir Bin Said alisema Uongozi wa Jumuiya ya Taassi
hiyo unafarajika na muitikio mkubwa wa wazazi na walezi waliooonyesha
katika kuipokea taasisi hiyo yenye mnasaba na mazingira yao.
Sheikh Nassir alisema juhudi
zitaendelea kuchukuliwa na Uongozi huo ili kuona malengo
yaliyokusudiwa ya kusaidia jamii kukabiliana na mazingira
yanayowazunguuuka yanafanikiwa vyema na kustawisha jamii zao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
18/1/2015.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni