Mwanafunzi aliyeongoza kwa kufanya
vizuri katika mtihani wa kidato cha nne kitaifa mwaka jana, Nyakaho
Marungu akipongezwa na mama yake Celestina Maro, nyumbani kwao
Kitunda Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya Baraza la Mitihani la
Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya mtihani huo.
Na Mwandishi Wetu
Ufaulu katika matokeo ya mtihani wa
kidato cha nne umeongezeka kwa asilimia 10, chini kidogo ya viwango
vya Matokeo Makubwa Sasa (BRN), lakini shule za Serikali za vipaji
maalumu, kongwe na za seminari zimeendelea kuporomoka.
Katika matokeo hayo, Shule ya
Sekondari ya Kaizirege ya mkoani Kagera, iliyoanzishwa mwaka 2010,
ndiyo imekuwa kinara ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio baada ya mwaka
jana kushika nafasi hiyo lakini kwa upande wa shule zenye watahiniwa
chini ya 40. Shule iliyoshika mkia ni Manolo iliyopo Tanga, mkoa
ambao umetoa shule tano miongoni mwa shule zilizoshika nafasi 10 za
mwisho.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu
kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji wa Wastani kwa Kutumia
Pointi (GPA) ambao unaonyesha shule zote 10 za kwanza ni za binafsi.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini
Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta), Dk. Charles Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni
wanafunzi 196,805 sawa na asilimia 68.33 ya watahiniwa 288,247
waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na 235,227, sawa na asilimia
58.25 ya waliofaulu mwaka 2013.
Dk. Msonde alisema wavulana
waliofaulu ni 106,960 sawa na asilimia 69.85 na wasichana ni 89,845
sawa na asilimia 66.61.
Kwa mujibu wa maelekezo ya BRN,
ufaulu wa upande wa sekta ya elimu, ambayo ilipangiwa malengo tisa,
ulipaswa uwe asilimia 70.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni