Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akitoa
taarifa ya mkutano wa wawekezaji (Round Table Investment Forum) na
wakuu wa nchi 5 za ukanda wa Afrika Mashariki utakaofanyika jijini
Dar es Salaam kuanzia Machi 25 hadi 26 mwaka huu.
Kamishina wa Polisi wa Kanda Maalum ya
Dar es salaam Suleiman Kova akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na
usalama katika jiji la Dar es salaam na vifo vya watu 7 waliopoteza
maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa
zinazoendelea kunyesha katika jiji la Dar es Salaam.
Na Aron Msigwa –MAELEZO.
Akitoa taarifa ya mkutano huo Mkuu wa
wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki amesema kuwa Marais
hao Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Yoweri
Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Joseph Kabila wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watahudhuria mkutano huo wakiwa
wameambatana na jumla ya wawekezaji 350.
Amesema Tanzania kwa mara nyingine
imepata heshima ya kuandaa mkutano huo na kufafanua kuwa wawekezaji
hao wamekwisha anza kuwasili jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 22
, huku marais nchi hizo wakitarajiwa kuwasili jijini humo kuanzia
Machi 24,2015.
Amesema wakiwa nchini Tanzania Marais
hao watashiriki kwenye mkutano wa wawekezaji utakaofanyika ukumbi wa
Mikutano wa Kimataifa Mwalimu J.K.Nyerere kuanzia Machi 25 hadi 26,
watatembelea bandari ya Dar es Salaam ili kuona namna nchi za Ukanda
wa Afrika Mashariki zinavyoshirikiana katika masuala ya ushuru wa
forodha na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Amebainisha kuwa kabla ya kuaondoka
nchini Tanzania Machi 26, 2015 Marais hao pia watatembelea
miundombinu ya reli inayotumika kusafirisha mizigo nchi za maziwa
makuu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika usafirishaji wa
bidhaa mbalimbali baina ya nchi zao.
KUHUSU MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA
JIJINI DAR ES SALAAM
Aidha, kuhusu mvua zinzoendelea
kunyesha katika jiji la Dar es salaam na kusababisha madhara, Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amewataka wananchi
kuzingatia agizo la kuhama mabondeni na maeneo mengine hatarishi ili
waepuka maafa kufuatia watu 7 kupoteza maisha kutokana na kutokana na
athari za mvua zinazoendelea kunyesha.
Akifafanua kuhusu matukio hayo Mhe.
Sadiki amesema maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo na kupata maafa
hayo ni bonde la Mto Msimbazi na eneo la Buguruni kwa Myamani.
Amesema kuwa maeneo yaliyokumbwa na
mafuriko hayo yameonekana kuwa na wingi wa takataka ngumu na wingi
wa mifuko ya plastiki iliyotupwa na wakazi hao hali iliyochangia
kuziba mifereji inayopeleka maji katika bonde la mto Msimbazi na maji
hayo kuhamia kwenye makazi ya watu.
Ameeleza kuwa kazi ya uokoaji , kumwaga
dawa kwenye maji yaliyotuama ili kuzuia athari ya magonjwa ya
milipuko, kuzibua mifereji na kukusanya taka katika maeneo hayo
inaendelea ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kuwataka wakazi
hao kuepuka kutupa taka ngumu zinazoziba mifereji ya maji.
Amesema Serikali inasubiri taarifa
kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa kwa maeneo ambayo wakazi
wake wanaishi kihalali ili waweze kupatiwa misaada ya kibinadamu.
Kwa upande wake Kamishina wa Polisi wa
Kanda Maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova amethibitisha vifo vya
watu hao 7 waliopoteza maisha kutokana na maeneo yao kukumbwa na
mafuriko pamoja na athari ya Umeme.
Akitoa ufafanuzi wa vifo hivyo amesema
kuwa watu 5 wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji na wengine 2
wamepoteza maisha kutokana na ajali iliyosababishwa na Lori moja
kugonga Transfoma ya umeme eneo la Buguruni Mnyamani.
Kamishna Kova amesema tayari Jeshi la
Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na Shirika
la Ugavi wa Umeme (TANESCO) wameunda kikosi kazi cha uokoaji.
Ametoa wito kwa madereva wa magari ya
mizigo, mgari binafsi na yale ya abiria kuepuka kupita katika maeneo
yaliyojaa maji ili kuepuka ajali na vifo vinavyoweza kuzuilika.


Hakuna maoni :
Chapisha Maoni