Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed akitoa maelezo kwa wandishi wa Habari Ofisini kwake Vuga kuhusu kilele cha madhimisho ya Sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar yatakayo adhimishwa kesho Januari 12 kiwanja cha Amani. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Na Khadija Khamis – Maelezo
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema imeweka ulinzi wa kutosha katika maeneo yote ya Zanzibar ili kuhakikisha sherehe hizo zinafanyika katika hali ya amani na usalama mkubwa.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed huko Ofisini kwake Vuga wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali .
Amesema Serikali haitomvumilia mtu yeyote mwenye nia mbaya ya kuharibu sherehe hizo na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa mtu atakaeonekana na dalili za kufanya vitendo vya kuhatarisha amani na usalama
Alisema kuwa kesho ni kilele cha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo wazee walijitoa muhanga kuikomboa nchi kutoka mikononi mwa wakoloni kwa nia ya kuleta umoja amani upendo na maendeleo ya nchi .
“Mapinduzi yetu ni halali hivyo tutaendelea kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi yetu kwa maslahi yetu na ya vizazi vyetu”.Alisema Waziri Aboud.
Alifahamisha kuwa kumeandaliwa utaratibu maalum wa kuwasafirisha Wananchi kutoka Mikoa yote ya Unguja na Pemba ili waweze kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo.
Alieleza kuwa sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na wageni mbali mbali mashuhuri wakiwemo Mabalozi wa Nchi za nje waliopo Tanzania na viongozi wa kitaifa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Alisema katika sherehe hizo kutakuwa na maandamano ya wananchi wa Mikoa mitano ya Unguja na Pemba Wafanyakazi wa Taasisis za Serikali pamoja na Wanafunzi wa Vyuo na Skuli mbali mbali za hapa Zanzibar .
Waziri Aboud alisema kuwa katika kudumisha Mapinduzi, Gwaride rasmi la vikosi vya ulinzi na usalama na vikosi vya Idara maalum vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar vinatarajiwa kushiriki na burudani ya ngoma za asili kutoka Unguja na Pemba zitatumbuiza .
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni