Mkurugenzi
Miradi wa Kamuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Miundombinu ya Ujenzi ya
Garware ya Nchini India Bwana Deepak Menghnani kati kati akizungumza
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika
Hoteli ya Kimataifa ya Eros Mjini New Delhi India, kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Kampuni ya Garware
Bwana Jatindery V. Sehgal.
Mkurugenzi wa
Miradi wa Kampuni ya Garware Bwana Deepak Mnghnani Kushoto akifafanua
jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi aliyekaa kati kati na wa kwanza kulia ni Mjumbe
wa Bodi ya wadhamini ya Kampuni ya Gaware Bwana Jatindery V. Sehgal.
Balozi Seif Ali
Iddi wa Pili kutoka Kulia akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa
Kampuni ya Garware mara baada ya kumaliza mazungumzo yao katika
Hoteli ya Kimataifa ya Eros Mjini New Delhi India, wa kwanza kutoka kulia ni Mkurugenzi
wa Miradi wa Kampuni ya Garware Bwana Deepak Mnghnani na kulia ya
Balozi Seif ni Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Kampuni ya Gaware Bwana
Jatindery V. Sehgal pamoja na Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India
Balozi Mohamed Hija Mohamed.
Picha na –OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa
miundombinu ya Ujenzi ya Garware yenye Makao Makuu yake Mjini Bumbay
Nchini India imeonyesha nia yake ya kutaka kujenga Ukumbi Mpya wa
Kisasa wa Kimataifa wa Mikutano Zanzibar endapo itapata fursa ya
kufanya kazi hiyo.
Uwamuzi huo umekuja kufuatia
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na mpango wa Kutaka kujenga
Ukumbi wenye hadhi hiyo katika azma yake ya kuimarisha Sekta ya
Utalii inayoonekana kuimarika na kuleta ufanisi mkubwa.
Mkurugenzi Miradi wa Kamuni Garware
Bwana Deepak Menghnani alithibitisha hilo wakati wa mazungumzo yake
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mwishoni
mwa ziara ya Wiki Moja ya Ujumbe wa Zanzibar hapo katika Hoteli ya
Kimataifa ya Eros Mjini New Delhi India.
Bwana Deepak Menghnani
alimthibitishia Balozi Seif kwamba Wahandisi wa Kampuni ya Garware
iliyoanzishwa karibu miaka sita iliyopita wana uwezo wa Kujenga Jengo
la Mikutano katika kipindi kisichozidi miaka Mitatu kwa mujibu wa
uwezo wa mahitaji ya muhusika.
Alisema teknolojia rahisi
inayotumika katika Kampuni hiyo imewawezesha Wataalamu na Wahandisi
wake kuendesha ujenzi wa Mjengo tofauti ikiwemo Hospitali, Skuli,
Ofisi za Serikali na hata Taasisi Binafsi pamoja na nyumba za Makaazi
kwa bei inayomuwezesha mtu wa kawaida kumudu kununua.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya
Kimataifa ya Uhandisi wa miundombinu ya Ujenzi ya Garware alimueleza
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi hiyo ya ujenzi
imekuwa ikishirikiana na Wahandisi waliobobea kutoka Nchini Misri ili
kuiwezesha kuwa na uhimili wa Kimataifa.
Bwana Deepak Menghnani alisema
Garware tayari imeshatoa huduma za ujenzi katika Mataifa ya
Bukinafaso,Sri Lanka na Dubai ndani ya kipindi cha miaka Minane tokea
kuanzishwa kwake.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar iko tayari kuuandalikia barua ya mualiko Ujumbe wa Viongozi
wa Kampuni hiyo katika muda mfupi ujao ili kujionea mazingira ya
Zanzibar na kuona hatua gani zinastahiki kuchukuliwa katika mwanzao
wa kuelekea kwenye mpango huo wa ujenzi wa Ukumbi wa Kimataifa.
Balozi Seif alisema Zanzibar
imeshafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika uimarishaji wa Sekta ya
Utalii lakini kinachokosekana kwa wakati huu ni uwepo wa Ukumbi wa
Kimataifa unaotoa fursa kwa Wageni na hata Nchi rafiki kuelekeza
nguvu zao za kufanya makongamano, Mikutano na hata Vikao vya
Kimataifa.
“ Zipo kumbi za Mikutano
zinazotumika katika baadhi ya Mahoteli Mjini na sehemu za Vijijini
Zanzibar lakini hazikidhi mahitaji halisi kutokana na udogo wake ”.
Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema ipo mikutano na
baadhi ya semina za Kimataifa zinazopangwa kufanyika Visiwani
Zanzibar lakini wajumbe wa Mikutano hiyo hulazimika kuishi mbali na
maeneo yao ya mikutano jambo ambalo huleta usumbufu wa kujipangia
mambo yao mengine binafsi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi amemaliza ziara yake Nchini India na sasa
amewasili Dubai kwa Mapumziko mafupi ya siku mbili na baadae atarejea
Nchini Tanzania kuendelea na majukumu yake.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
26/3/2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni