Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC
Tanzania Bw. Edward Marks, akizungumza jambo wakati wa maadhimisho
ya Benki yake kutimiza miaka 50, tukio lililofanyika Mjini Dodoma
Jana usiku.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
Benki ya NBC, Bw. Nehemiah Mchechu, akitaja mafanikio makubwa
yaliyofikiwa na Benki hiyo, wakati wa uzinduzi rasmi wa maadhimisho
ya Benki hiyo kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, tukio
lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Morena, Mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Josephat Kandege, akipokea tuzo
kwaniaba ya wabunge, tuzo iliyotolewa na NBC kutambua mchango wa
Bunge katika kuanzishwa kwa Benki hiyo miaka 50 iliyopita.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb), akionyesha alama ya dole! akifurahia gawiwo
la shilingi bilioni 1.7 zilizotolewa na NBC kwa Serikali, ambayo
inamiliki asilimia 30 za hisa katika Benki hiyo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb), akishukuru baada ya kupokea gawiwo la
shilingi bilioni 1.7 zilizotolewa na NBC kwa Serikali, ambayo
inamiliki asilimia 30 za hisa katika Benki hiyo.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Samwel
Malecela, akitoa neon la shukurani kwenye hafla ya Benki ya Taifa ya
Biashara (NBC) kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, sherehe
zilizofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Morena mjini Dodoma. (Picha zote na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa
mara ya kwanza imetoa gawiwo la shilingi bilioni 1.7 kwa Serikali
ambayo inamiliki asilimia 30 ya hisa za Benki hiyo.
Hundi kifani ya kiasi hicho cha
fedha alikabidhiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Mpango (Mb), kwaniaba ya Waziri Mkuu, katika tukio la Benki hiyo
kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, tukio lililofanyika
katika Hoteli ya Morena Mjini Dodoma.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Benki
hiyo kutoa gawiwo kwa wanahisa wake katika kipindi cha miaka 9 baada
ya kuanza kupata faida ya uwekezaji wake hapa nchini.
Dkt. Mpango aliishukuru Benki hiyo
kwa kuanza kutoa gawiwo kwa wanahisa wake baada ya ukame wa muda
mrefu na kuelezea matumaini yake kwamba kiasi cha gawiwo kitaongezeka
zaidi miaka ijayo.
Hata hivyo alizitaka Benki zote hapa
nchini kupunguza riba za mikopo inazotoza kwa wateja wao hasa baada
ya Benki Kuu ya Tanzania-BOT kupunguza riba za mikopo kwa mabenki
kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12.
Alizitaka pia taasisi za fedha
nchini, kuwekeza fedha katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa
Maendeleo kwa njia ya mikopo kwa wateja wao kwa ajili ya ujenzi wa
viwanda vitakavyosisimua uchumi na kukuza ajira nchini.
Alipongeza pia juhudi zilizofanywa
na Benki hiyo kufanya uwekezaji mkubwa kwenye mtandao wa malipo ya
kielektroniki ikiwa ni maagizo ya Serikali kwamba malipo yote ya
Serikaloi yafanyike benki au kupitia miamala ya kielektroniki
“Nimefurahi kuthibitishiwa kwamba,
kutoka tarehe 1 Julai 2016 hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2017, NBC
imekusanya fedha za Serikali na kuzituma kielektroniki katika Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) jumla ya Shillingi Billioni 991” aliongeza
Dkt. Mpango.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Benki hiyo, Nehemiah Mchechu, alieleza Mkakati wa Benki hiyo ya tatu
kwa ukubwa hapa nchini ikitanguliwa na Benki za NMB na CRDB, huku
ikiwa imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1, kwamba
imejipanga kusogeza huduma zake kwa wananchi na wafanyabiashara wa
kati na wa chini kabisa.
“Mwaka jana Benki yetu imepata
faida ya zaidi ya shilingi bilioni 13 na katika mkutano Mkuu wa
wanahisa tuemekubaliana kutoa gawiwo kwa wawekezaji” aliongeza Bw.
Mchechu.
NBC inamilikiwa na wabia watatu,
wakiwemo kundi la Mabenki ya Barclays (ABSA Group ltd) ya Afrika
Kusini, inayomiliki hisa nyingi zaidi, Serikali ya Tanzania yenye
hisa asilimia 30 huku Benki ya Dunia kupitia Taasisi yake ya Fedha
ijulikanayo kama The International Finance Corporation (IFC), ikiwa
na hisa asilimia 15.
Mwisho
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni