Wadau wa Tasnia ya Korosho wakimsikilza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wawa Dau wa Tansnia ya Korosho Nchini ambao umefunguliwa na Waziri Mkuu May 13, 2017 katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango Mkoani Dododm. (PICHA NA OWM).
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*Serikali kugawa salpha bure kwa
wakulima wa korosho
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkurugenzi wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuhakikisha
wanafanya marekebisho ya mizani katika maghala ya kuhifadhia korosho
ili kuepuka changamoto ya kutofautiana kwa uzito wa bidhaa hiyo kila
inapofikishwa kutoka katika vyama vya msingi.
Amesema kitendo cha mizani za kwenye
maghala hayo kupunguza uzito wa korosho zinazopelekwa kutoka kwenye
Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) hakivumiliki, hivyo Wakala wa
Vipimo ipendekeze aina ya mizani zitakazotumika katika upimaji wa
korosho.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumamosi, Mei 13, 2017) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa
Wadau wa Tasnia ya Korosho uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha
Mipango mjini Dodoma.
“Kuna jambo baya sana linaendelea
kila korosho inayofikishwa katika ghala kuu lazima kilo ziwe
zimepungua kwa zaidi ya kilo mia moja mpaka elfu, kwa nini korosho
tani kumi zikiletwa kwenye mizani yenu zinasoma tani nane kwa nini?
“Na huwa haitokei ikasoma tani
kumi na mbili, wakati wote huwa inasoma chini tu, watu wa WMA mpo
fanyesni marekebisho, haiwezekani tukavumilia wizi huu. Huna mkorosho
hata mmoja lakini mwaka huu utasikia umeuza tani zaidi ya elfu tano.
Jambo hili lisijitokeze tena,”
amesisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali
imeendelea kuimarisha na kuboresha utaratibu wa stakabadhi ghalani na
kupambana na biashara ya kangomba, hivyo viongozi wa Mikoa inayolima
korosho wahakikishe wanawashughulikia watu wote watakaobainika
kushiriki kwenye biashara hiyo bila ya kujali wadhifa wao.
Amesema mwelekeo wa Serikali kwenye
sekta ya kilimo ni kuhakikisha kuwa kilimo kinakuwa sehemu muhimu ya
kuimarisha uchumi, kuongeza kipato cha mkulima na kuchochea ukuaji wa
viwanda ili kuongeza ajira.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba amesema takwimu zilizotolewa na
Benku Kuu ya Tanzania (BoT) mwezi Februari mwaka huu, zinaonyesha
zao la korosho linaongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Zao
la korosho limeliingizia Taifa Dola milioni 346.6, likifuatiwa na
zao la tumbaku dola 276 na kahawa dola 152.9.
“Zao la korosho linakuwa zao kuu
la biashara nchini na tayari mikoa ya Dodoma, Morogoro, Iringa,
Njombe na Mbeya imeanza kulima, hivyo kuongeza idadi ya mikoa
inayolima zao hilo nchini na kufikia 11 na wilaya 40,” amesema.
Aidha, Dkt. Tizeba ameitaka Bodi ya
Korosho Tanzania (CBT) kuhakikisha inakuwa makini na viuatilifu
vinavyoingizwa nchini kwa kuvipima kwa kutumia wataalamu wa Serikali
ili kujiridhisha ubora wake kabla ya kuwafikishia wakulima.
Pia Dkt. Tizeba amesema katika msimu
wa mwaka huu Serikali itagawa salpha bure kwa wakulima wa zao la
korosho kwa ajili ya kupuliza kwenye mikorosho yao ili isishambuliwe
na wadudu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, MEI 13, 2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni