Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia), akitoa maelekezo
wakati alipokagua ujenzi wa Jengo la ghorofa 5 la Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) mjini Dodoma, kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa NBS
Dkt. Albina Chuwa na kushoto kwake ni Mhandisi Mshauri Bw. Abdulkarim
Msuya.
Mhandisi Mshauri na Msimamizi wa
ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma, Mhandisi
Abdulkarim Msuya, akimwonesha Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), mfumo wa kupoza hewa, alipotembelea ili
kukagua ujenzi wa Jengo la NBS mjini Dodoma, ambalo litagharimu
shilingi bilioni 11.6.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), (wa pili kulia), akipata maelezo ya ujenzi
wa Makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu mjini Dodoma,
alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa 5 ambalo
hadi kukamilika litagharimu shilingi bilioni 11.6.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), akisaini kitabu cha wageni alipotembelea
eneo la ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mkoani Dodoma.
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), amekagua ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu-NBS mjini Dodoma na kutoa wito kwa wakandarasi wanaojenga
miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo kutumia malighafi
zinazozalishwa hapa nchini ili kuongeza mapato ya Serikali na
kuchochea ukuaji wa uchumi.
Amesema hayo baada ya kushuhudia
mkandarasi anayejenga jengo hilo Hainan International Ltd ya China,
akitumia vifaa mbalimbali vya ujenzi vinavyopatikana hapa nchini
zikiwemo mbao na vifaa vya umeme, hatua ambayo amesema inachangia
kuwaongezea kipato wananchi.
Akizungumzia ujenzi huo, Dkt. Mpango
amesema jengo hilo litatumika ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa
kwakuwa litatumika kuchakata takwimu mbalimbali zitakazotumika katika
kutunga sera na mipango mbalimbali ya kuendeleza nchi.
“Huwezi kupanga mipango yoyote
bila kuwa na takwimu nzuri na bora, hapa ndipo vile “vichwa”
vyetu vya takwimu nchini vitachakata takwimu hizo ndipo zitumike
katika kutunga sera bora kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu”
Alisistiza Dkt. Mpango
Dkt. Mpango alielezea furaha yake
kwamba jengo hilo linajengwa mjini Dodoma badala ya Dar es Salaam
ambako lilikuwa lijengwe ili kusukuma azma ya Serikali ya kuhamia
Dodoma kwa kuhakikisha miundombinu muhimu zikiwemo ofisi
vinapatikana.
Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa jengo
hilo lenye ghorofa 5, umetoa ajira kwa zaidi ya vijana 120 kutoka
sehemu mbalimbali nchini hatua ambayo amesema imewafanya vijana wengi
kujipatia kipato cha kujikimu maisha yao.
Dkt. Mpango ameupongeza uongozi wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kwa kazi nzuri wanayoifanya ya
ujenzi wa ofisi mpya katika Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma
inayojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, Mashirika
ya Maendeleo ya Kimataifa ya Canada na Uingereza kwa kushirikiana na
Serikali.
Kwa upande wake Mtaalam Mshauri na
Mdhibiti Viwango anayesimamia ujenzi wa jengo hilo Mhandisi
Abdulkarim Msuya amesema kuwa jengo hilo lenye thamani
ya shilingi bilioni 11.6
linatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwakani.
Amesema kuwa ujenzi huo umefikia
hatua za mwisho kwa asilimia 82 ambapo asilimia 18 zilizobaki ni za
umaliziaji na kwamba mkandarasi aliyepewa kazi hiyo anatarajia
kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku 30 hadi 45 kuanzia sasa.
Mwisho
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni