Mahafali ya saba ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar Es Salaam
imefanyika wiki iliyopita jijini DSM ikihudhurisha wahitimu zaidi ya 500 katika
ngazi ya Astashahada, Stashahada na
Shahada ya juu.
Taasisi ya Teknologia ya Dar Es Salaam, DIT ambayo zamani
ilikuwa ikijulikana kama Chuo cha Ufundi cha Dar Es Salaam, maarufu kama Dar
Tech, inayo Idara 8 kama ifuatavyo, Idara ya Uhandisi Kompyuta, Idara ya Uhandisi
Ujenzi, Idara ya Uhandisi Migodi, Idara ya Uhandisi Umeme, Idara ya Uhandisi
Elektroniki na Mawasiliano ya Anga, Idara ya Uhandishi Mitambo, Idara ya
Sayansi na Teknologia ya Maabara, Idara ya Teknologia ya Habari.
Wahitimu kutoka Idara mbalimbali walitunukiwa Vyeti,
Diploma, na Shahada ya juu kulingana na masomo waliyochukua.
Mgeni Rasmi katika Hafla hiyo alikuwa Mheshimiwa Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbaraw, Mbunge akimuwakilisha Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal, ambaye alikuwa na udhuru.
Maandamano ya mahafali yalianza saa 7.30 mchana kwa Wahitimu
kuingia viwanja vya michezo katika Taasisi hiyo, na Mgeni Rasmi aliwasili muda
wa saa 8.00 akiongozana na jopo na Wahadhiri pamoja na Mkuu wa Taasisi Profesa
John Kondoro.
Baada ya Mlau [Chief of Protocol] kutoa salamu za
makaribisho, na kusimika Rungu rasmi katika meza iliyoandaliwa kama inavyofanya
katika ukumbi wa Bunge, Wimbo wa Taifa uliimbwa na baadae Mkuu wa Taasisi
alisoma hotuba yake, ikifuatiwa na hotuba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya
Teknolojia ya Dar Es Salaam ambaye ndie aliyemkaribisha Mgeni Rasmi kusoma
hotuba yake na baadaye zoezi la kutunuku Vyeti kuanza.
Wahitimu wa ngazi ya cheti [Astashahada] katika fani ya
Ufundi wa Teknolojia ya Habari yaani Basic Technician Certificate in
Information Technology, ndio waliokuwa wa kwanza kutunukiwa wakifuatiwa na
Idara zingine, na hatimaye kumalizia na Wahitimu wa Shahada ya Juu.
Wahitimu 49 wa fani ya Uhandisi Ujenzi, yaani Bachelor of
Engineering in Civil Engineering ndio waliokuwa wa kwanza kutunukiwa Shahada ya
juu wakifuatiwa na 24 wa fani ya
Uhandisi Kompyuta yaani Bachelor of Engineering in Computer Engineering.
Wahitimu wote wa Shahada ya Juu mara baada ya kutunukiwa
Shahada zao walivaa rasmi kofia zao kuashiria kwamba sasa ni wahitimu kamili,
huku brass band ya Jeshi la Magereza wakipiga wimbo maalum wa fan fair wakati
wahitimu kutoka Idara mbalimbali wakitajwa majina yao na kuinuka katika viti
vyao na kujipanga mbele ya Jukwaa la Mgeni Rasmi kupokea tuzo hizo.
Zoezi la mwisho lilikuwa ni kutangazwa rasmi kwa Wahitimu
bora wa kila Program na Idara wanazotoka. Upande wa Stashahada walikuwa
wahitimu 8 wote wa jinsia ya kiume, na upande wa Shahada waliotunukiwa walikuwa
wahitimu 5 wanne wakiwa ni wanaume na mmoja ni msichana aliyetambulika kwa jina
la Cecylia Kuguru, ambaye alishangiliwa na ukumbi mzima uliokuwa umefurika na
wazazi, walezi, wanafunzi pamoja na wageni waalikwa.
Mgeni Rasmi Profesa Makame Mbarawa kwa Mamlaka aliyopewa
alitangaza hapo hapo kumpa scholarship
ya kusoma Masters Degree mhitimu huyo katika Chuo chochote
atakachopenda.
Tamko hilo liliongeza vifijo na nderembo uwanjani hapo huku
Mgeni Rasmi akiwahimiza wanafunzi wengine kusoma kwa bidii, kuwa wanafunzi bora
na hatimaye kujipatia nafasi kama hizo za kusomeshwa bure na Serikali.
Mhitimu Cecylia Kuguru anatokea Idara ya Uhandishi
Elektroniki na Mawasiliano Anga, mafunzo ambayo yanamuwezesha kupata ajira na
nafasi ya Juu katika Idara ya Mawasiliano ya angani kama Control Tower ya
Mawasiliano ya ndege, meli na kadhalika.
Mwanafunzi Mhitimu bora ndugu Elias Eliud kwa niaba ya
wahitimu wenzake alitoa neno la shukrani, na baadaye sherehe zilifungwa kwa
kupigwa picha za pamoja Wahitimu bora na Mgeni Rasmi, Wakuu wa Idara pamoja na
Wageni Waalikwa.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni