Jumamosi, 1 Machi 2014
SHIRIKISHO LA MADINI THAILANDKUISAIDIA TANZANIA KUWA KITIVO CHA MADINI AFRIKA
Na Asteria Muhozya, Bangkok,
Kutokana na kuwa na hazina kubwa ya madini ya aina mbalimbali hususani madini ya vito na usonara tofauti na nchi nyingi za Kiafrika, yakiwemo madini ya Tanzanite, Shirikisho la madini ya vito na usonara la Thailand, limehaidi kuisaidia Tanzania kuikuza sekta hiyo, katika nyanja za kibiashara na kiuchumi ili kuifanya Tanzania kuwa, kitivo kikubwa cha madini barani Afrika, huku ikianzia na kuboresha maonesho ya kimataifa ya madini ya vito na usonara ya Arusha yanayofanyika kila mwaka.
Aidha, nia ya shirikikisho hilo imetokana na uwepo wa makampuni mengi ya wafanyabiashara wa Thailand kupenda madini yanayotoka Tanzania ikiwa pia ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Thailand.
Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti na Viongozi wa Shirikisho la madini ya vito na usonara Thailand na kiongozi kutoka Idara ya Ukuzaji Biashara ya Kimataifa katika Wizara ya Biashara ya Thailand.
“Tunataka kuisaidia Tanzania kutengeneza fursa nyingi zaidi za kibiashara katika tasnia hii. Tanzania ina kila sababu ya kufanikiwa katika hili, kuna madini mengi na bora ya kuifanya kuwa kituo kikubwa cha madini Afrika”. Amesema Tom Broke, Makamu wa Rais wa Shirikisho la madini ya Vito na usonara Thailand.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Ukuzaji Biashara ya Kimataifa katika Wizara ya Biashara ya Thailand, Bibi Nuntawan Sakuntanaga, ambaye amelitembelea banda la Tanzania na kufurahishwa na aina za madini zilizowasilishwa, amehaidi kuboresha maonesho hayo ili kuziwezesha nchi zenye hazina kubwa kama Tanzania kuweza kushiriki maonesho hayo kwa kiwango kikubwa.
“Tanzania inashiriki katika maonesho haya kwa mara ya kwanza, tunataka kuwasaidia katika hili, ili muweze kujenga mtandao mkubwa zaidi wa kibiashara kwasababu mna kila sababu ya kufanikiwa kutokana na umuhimu wenu katika sekta hii. Sisi sote tunawahitaji ninyi.” Amesema Bibi. Sakuntanaga.
Hivyo, amewataka wafanyabiashara wa Kitanzania kujenga mtandao wa kibiashara na wadau wengine duniani kutokana na ubora wa madini yanayopatikana nchini.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania, (TAMIDA) Bw. Sam Mollel, amewaomba viongozi wa Shirikisho hilo kuhakikisha kuwa wanaboresha mazingira ya kibiashara kati ya Tanzania na Thailand ili kuwawezesha wafanyabiashara wa madini kushiriki kwa wingi na kuleta bidhaa nyingi zaidi katika maonesho mengine nchini humo ikiwemo kufanya biashara na Thailand.
Kwa upande wake kamishna Msaidizi Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Hamis Komba, ameeleza kuwa, jambo hilo ni fursa kubwa kwa Tanzania na wadau wa madini nchini ambayo wanahitaji kuitumia kikamilifu kutokana na nafasi kubwa ambayo Tanzania imepewa katika maonesho hayo na utayari wa nchi ya Thailand kutaka kushirikiana na Serikali na wafanyabiashara wa madini wa Tanzania.
Ameongeza kuwa, maonesho ya madini ya Arusha ni fursa nyingine kwa Tanzania kutokana kuwa nchi pekee katika ukanda wa Afrika, ambayo inafanya maonesho ya vito vya madini na usonara, Afrika.
“Tumejidhatiti kujifunza kutoka kwao na tumefarijika kuona namna wafanyabiashara mbalimbali wanavyothamini madini yetu na maonesho yetu ya Arusha. Hiyo ni hatua ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha madini”. Amesema Kamishna Komba.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)



Hakuna maoni :
Chapisha Maoni