Mwakilishi wa Kikundi cha wajasiri amali wa usafirishaji abiria kwa njia ya Bahari cha Rehema za Mungu cha Kisiwa cha Tumbatu Wilaya ya Kaskazini “ A “ akipokea hundi ya shilingi Milioni 2,400,000/- kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi zilizotolewa na Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi Zanzibar.
Mwakilishi wa Kikundi cha wajasiri amali CHA Uvivu si Mtaji cha Tunguu Wilaya ya Kati akipokea hundi ya shilingi Milioni 2,000,000/- kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi zilizotolewa na Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi wa Vikundi 12 vya wajasiri amali wa Kisiwa cha Unguja wakifuatilia hafla ya utowaji Mikopo kwa vikundi vyao kutoka mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iliyofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto Mwanakwerekwe.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kati kati waliokaa vitini akiwa katika Picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Vikundi 12 vya ujasiri amali wa kisiwa cha Unguja waliopata Hundi ya mkopo wa kuendeleza Miradi yao.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohammed na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi.
Kushoto yake Balozi ni Mwenyekiti wa Kamati ya kuchangisha Fedha za Mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Mh. Haroun Ali Suleiman na Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Wanawake na Watoto Mh. Mgeni Hassan Juma.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Vikundi 12 vya wajasiriamali wa miradi tofauti ya Maendeleo katika Wilaya sita za Kisiwa cha Unguja wamekabidhiwa hundi za mikopo kutoka Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi ulioanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mfuko huo wenye lengo la kuwakomboa Wananchi hasa wanawake, Vijana pamoja na wanafunzi waliomaliza mafunzo yao ya sekondari na Vyuo ulizinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein Tarehe 21 mwezi Disemba mwaka 2013.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi hundi hizo kwa wawakilishi wa vikundi hivyo kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar hapo Makao Makuu ya Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mwanakwerekwe Nje Kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Jumla ya shilingi Milioni 36,500,000/- zimetolewa na mfuko huo kukopeshwa wajasiri amali hao wa Unguja ambapo baadaye wiki hii watapatiwa wale wa Kisiwani Pemba ili kuendesha miradi yao ya kiuchumi kwa lengo la kupunguza umaskini na kujipatia kipato.
Akizungumza na wajasiri amali hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Wananchi, hasa Akina mama na Vijana waliomaliza masomo yao ya sekondari na vyuo vya elimu ya juu kuchangamkia fursa inayotolewa na Serikali ya kuwapatia mikopo itakayowawezesha kutekeleza vyema miradi yao ya kiuchumi na hatimae kujiajiri wao wenyewe.
Balozi Seif alisema Serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa Uwezeshaji ili kutoa mikopo nafuu kwa Wananchi wake licha ya kuwepo kwa Taasisi nyingi za kifedha zinazotoa mikopo mbali mbali kwa wajasiri amali lakini bado wananchi wachache ndio wanaofadika na mikopo ya taasisi hizo.
Alisema ukweli huo ndio changamoto kubwa ililoipa Serikali kwa kuimarisha Taasisi hiyo maalum itakayoyalenga makundi hayo ili kuyasaidia kukabiliana na tatizo la mitaji ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi na maendeleo.
Hata hivyo Balozi Seif aliwatahadharisha wananchi wanaopatiwa na wale watakaopatiwa mikopo hiyo waelewe kwamba fedha za mfuko huo sio sadaka kwani zinahitajika kurejeshwa ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kupatiwa mikopo hiyo.
“ Malengo na shabaha ya Serikali yetu ni kuwa na huduma endelevu za kutoa mikopo hasa ikilenga kwa wananchi walio Vijijini kupitia fursa hiyo. Azma hii haitofikiwa iwapo wakopeshwaji wataingia mitini baada ya kupata mikopo “. Alitahadharisha Balozi Seif.
“ Tutahakikisha kuwa jitihada za kuanzishwa kwa mfuko huu zinakwenda sambamba na juhudi kubwa za kusimamia utoaji wa mikopo yenyewe, udhibiti na urejeshaji wa fedha ili mfuko huu uwe endelevu na wananchi walio wengi waweze kufaidika na jitihada zetu “. Balozi Seif alikariri maneno ya Rais wa Zanzibar Dr. Sheni aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa mfuko huo Disemba 21 mwaka 2013.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka kuanzisha vipindi maalum vya Redio na Televisheni kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya namna bora ya kutunza fedha katika maisha yao ya kila siku.
Alisema taaluma hizo kwa kiasi kikubwa zinaweza kuwasaidia wakopeshwaji kutumia mikopo yao kama ilivyokusudiwa badala ya baadhi ya wahusika hao kutumia mikopo hiyo kwa masuala mengine.
“ Mikopo hii inapaswa kutumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na sio kuolea. Kununua dhahabu, au kujengea Nyumba kwa sababu mkopo huu unatakiwa kulipwa. Tunataka kukopa iwe harusi na kulipa pia iwe harusi badala ya kukopa kuwa harusi na kulipa ikawa matanga “. Alifafanua Balozi Seif.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kuzindua utoaji mikopo hiyo, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohammed aliwahakikishia wananchi kwamba huduma za mikopo nafuu zitapatikana katika kila shehia miongoni mwa shehia zote Unguja na Pemba.
Waziri Zainab alisisitiza kwamba kwamba Serikali itasimamia ipasavyo katika kuona matumizi mazuri ya fedha hizo yanafanywa na walengwa wanafaidika na mfuko huo wa uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
Alifahamisha kwamba Wizara hiyo imepokea maombi ya mikopo yapatao 433 na tayari 109 yameshafanyia tathmini ya kijumuisha vikundi 17 vingi vikiwa vya akina mama na Vijana.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Asha Abdulla alisema mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi tayari umeshakusanya shilingi Milioni Mia 972,140,000/- sawa na asilimia 95% ya lengo lililokusudiwa la kukusanya shilingi Bilioni Moja.
Katibu Mkuu Asha aliosema awamu ya kwanza ya mikopo hiyo inayofikia jumla ya shilingi Milioni 36,500,000/- unahusisha vikundi 12 ambapo kila wilaya imebahatika kupata vikundi viwili.
Mfuko wa uwezeshaji Wananchi kiuchumi umeanzishwa kwa mtaji wa shilingi Milioni 800,000,000/- zilizotokana na Mfuko wa Kujitegemea Zanzibar, Mifuko ya JK na AK pamoja na mkichango ya mashirika, Taaasisi jumuiya na Watu binafsi.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni