Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Nyumba NHC Bw. David Shambwe akisoma taarifa ya shirika hilo
kukanusha taarifa zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku na
mitandao ya kijamii kuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo Bw. Nehemia
Mchechu Kyando ameundiwa zengwe na baadhi ya wabunge ili aondolewe
katika shirika hilo, wanaofuaia katika picha ni Muungano Saguya Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Jamii, Bw. Martin Mdoe Mkuu wa Kitengo
cha Sheria na Benedict Kilimba Mkurugenzi wa Uendeshaji Miliki
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Nyumba NHC Bw. David Shambwe akisoma taarifa ya NHC kulia ni Mpnda
Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi.
Utangulizi:
Jumatatu na Jumanne ya wiki hii,
kumekuwa na taarifa zilizochapishwa kwenye moja ya gazeti la kila
siku zikieleza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Nehemia Kyando
Mchechu ameundiwa zengwe na Bodi ya Wakurugenzi ya NHC kwa nia ya
kuhakikisha kuwa harejeshwi tena katika wadhifa huo, hasa baada ya
Bw. Mchechu kumaliza muda wake wa kuliongoza Shirika hili.
Aidha, gazeti hilo liliwaaminisha
umma wa watanzania kuwa mizengwe hiyo inaungwa mkono na vigogo wa
Serikali wakiwemo Wabunge ambao kuwepo kwa Bw. Mchechu katika Shirika
kumewanyima ulaji ikiwemo kupangishwa nyumba za Shirika. Gazeti
lililienda mbali zaidi likidai kuwa Bw. Mchechu amewekewa masharti
magumu na Bodi hiyo ya kumtaka apunguze idadi ya Wakurugenzi wa
Menejimenti ya sasa ya Shirika.
Kwa kuwa habari hizo zimeleta
mtafaruku katika Shirika na zimesababisha umma kuwa na mijadala
mbalimbali juu ya jambo hili, tungependa kuwataarifu umma kuwa
taarifa hizo hazina ukweli wowote, na Shirika la Nyumba la Taifa
linapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
1. Kwanza, ifahamike kuwa Bodi ya
Wakurugenzi ya NHC ina miezi miwili tu tangu iteuliwe na Mamlaka
husika na haijawahi kukaa katika kikao chochote kujadili suala la
kumuondoa Mkurugenzi Mkuu na kupunguza Menejimenti ya Shirika iliyopo
sasa.
2. Tunapenda kuwafahamisha kuwa
Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti ya Shirika bado wana mikataba halali
ambayo haijamalizika muda wake, hivyo hoja ya kuwa Bwana Mchechu na
Menejimenti yake wanaundiwa zengwe baada ya kumaliza muda wao haina
ukweli wowote.
3. Kwamba kutokuwepo kwa Mkurugenzi
Mkuu kwenye ufunguzi wa miradi hakukutokana na kuwepo mizengwe kama
ilivyoripotiwa na Gazeti hili. Bw. Mchechu alikuwa katika likizo yake
ya mwaka iliyooanza tarehe 30 Juni na kumalizika Julai 18, 2014.
Likizo hii ni stahili halali ya Bw. Mchechu kama walivyo watumishi
wengine wa umma, na hakuichukua likizo hii kutokana na kuwepo
mizengwe ya kumuondoa kama ilivyoripotiwa na Gazeti hili. Kuanzia
tarehe 21 Julai, 2014 Bw. Mchechu yupo kikazi nje ya nchi na
anatarajiwa kuwa ofisini kwake tarehe 28 Julai, 2014.
4. Mwisho, tunapenda kuwatanabaisha
wanahabari kuwa kama ilivyo kawaida yetu, NHC imekuwa na itaendelea
kuwa mstari wa mbele kutoa habari makini kwa vyombo/chombo chochote
cha habari bila kuficha jambo lolote.
Hivyo, tunawaomba muendelee kuitumia
vyema fursa hii kupata habari zenye ukweli na zilizo sahihi kwa jambo
lolote mnalohitaji kuufahamisha umma wa watanzania. Kwa kufanya
hivyo, tutaendelea kuwa washirika wakubwa wa vyombo vya habari,
tukizingatia kuwa vyombo vya habari vina dhima na dhamana kubwa
katika kuleta tija kubwa kwa Shirika na Taifa letu.
Aidha, tunawafahamisha wateja wetu
kuwa hakuna mtafaruku wowote uliyopo ndani ya Shirika la Nyumba la
Taifa na kwamba tunaendelea kuwapa huduma zetu zilizo bora katika
sekta ya nyumba tuliyoaminiwa na Taifa kuisimamia.
IMETOLEWA NA:
BW. DAVID SHAMBWE,


Hakuna maoni :
Chapisha Maoni