Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda
ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya uongeze mapato yake ya ndani kwa
kuweka mifumo ya kisasa ya ukusanyaji mapato.
Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi,
Agosti 2, 2014) wakati akizindua stendi ya kisasa ya mabasi katika
eneo la Nane Nane nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
“Nikuombe Meya Kapunga, wewe na
watu wako ongezeni mapato ya ndani ya Jiji la Mbeya. Wekeni mifumo ya
kisasa ya makusanyo inayotumia teknolojia ya habari na mawasiliano,
acheni kutumia risiti za kuandika wa mikono,” alisema.
Akizungumzia mradi wa stendi mpya ya
mabasi, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa stendi hiyo ni miongoni mwa
kazi zilizo kwenye mradi mkubwa unaohusisha uboreshaji wa huduma na
miundombinu kwenye miji na majiji saba hapa nchini (Tanzania
Strategic Cities Programme).
Alisema mradi huo uliibuliwa na
Serikali tangu mwaka 2006 kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Miji na
majiji mengine yanayohusika na mradi huo ni Mwanza, Arusha, Tanga,
Kigoma, Mtwara na Dodoma.
“Utekelezaji wa miradi katika miji
na majiji haya saba, umetuwezesha kupata ufadhili katika awamu ya
pili ya mradi huu ambayo itajumuisha miji 17. Tusingekubaliwa kuingia
awamu ya pili kama ninyi madiwani msingesimamia vizuri miradi hii,”
alisema.
Akisoma taarifa ya mradi huo,
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Bw. Mussa Zungiza alisema ujenzi wa
stendi hiyo yenye ukubwa wa mita za mraba 30,000 utasaidia kupunguza
msongamano wa magari kwenye barabara kuu ya TANZAM ambako mabasi ya
mikoani yalikuwa yakisimama na kupakia ama kushusha abiria.
Alisema mradi huo wa stendi ya Nane
Nane uliogharimu sh. Bilioni 2.9/- ni sehemu tu ya mradi mzima ambao
thamani yake ni sh. Bilioni 31.4 ambazo zimetumika kujenga barabara
za kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 23.1, daraja moja na
dampo la kisasa la kutupia taka (sanitary land fill) katika kata ya
Nsalaga.
“Hata hivyo, mradi huo uko chini
ya uangalizi wa mkandarasi hadi Desemba 4, 2014 utakapokabidhiwa
rasmi kwa Halmashauri ya Jiji, “ alisema Bw. Zungiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya kuhakikisha unatengeneza
kwanza miundombinu ya maji na vyoo katika eneo jipya lililopo jirani
na stendi mpya ya Nane Nane ambalo limetengwa mahsusi kwa ajili ya
wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama ‘wamachinga’.
“Ni vema Jiji litenge kiasi cha
fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za muhimu kama maji na vyoo
badala kukimbilia kuwalundika mahali hapa. Wafanye biashara zao, na
hata mtu akitoka stendi akaja kununua bidhaa zao, kama na shida apate
mahali pa kujihifadhi,” alisema huku akishangiliwa na umati
uliohudhuria uzinduzi huo.
Aliwataka wawapangie maeneo ya
mabanda yao, na ikibidi watafute mwekezaji anayeweza kufanya kazi
hiyo. “Tusifanye kosa la kuja kuwalundika tu. Ni heri kugharimika
kidogo lakini pawe pazuri. Tengenezeni eneo hili ili kituo chenu kiwe
cha mfano na wengine waje waige,” aliongeza.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri
wa Nchi (OWM - Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, Balozi wa
Kenya nchini Tanzania, Bw. George Owuor, Kaimu Balozi wa Uganda
nchini Tanzania, Bibi Nora Katabarwa, Wakuu wa Mikoa ya Rukwa,
Iringa, Njombe na Katavi ambao walikuwa jijini Mbeya kuhudhuria
kongamano la Uwekezaji na wanahudhuria maonyesho ya Nane Nane Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni