Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akitia saini kitabu cha wageni mara
baada ya kuwasili Ofisi ya Wazazi CCM Wilaya ya Mjini kutekeleza
ahadi aliyoupa Uongozi Wa Jumuiya hiyo. Kushoto ya Mama Asha ni
Mwenyekiti wa Jumuiya Wazazi Wilaya ya Mjini Nd. Haji Lila.
Baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya
Wazazi CCM Mkoa na Wilaya ya Mjin walioshuhudia utolewaji wa vifaa
vya kazi za kiofisi vilivyotolewa na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi.
Mama Asha akizungumza na Viongozi
wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa na Wilaya ya Mjini hapo Miti Ulaya katika
hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya kazi za Kiofisi.
Mama Asha akikabidhi Kompyuta,
Printa na Mashine ya Foto Kopi kwa Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya
Mjini Nd. Haji Lila vitakavyotumika ndani ya Ofisi ya Wilaya hiyo
akitekeleza ahadi aliyowapa. Picha zote na Hassan Issa wa – OMPR –
ZNZ.
Press Release:-
Mambo na kazi kubwa inayoendelea
kufanywa na Chama cha Mapinduzi katika kusimamia utekelezaji wa Ilani
na Sera zake ndani ya Serikali zote mbili inapaswa kuelezwa na
hatimae ifahamike vyema kwa wananchi pamoja na jamii yote hapa
Nchini.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo katika hafla fupi ya
kukabidhi msaada wa vifaa vya Ofisi akitekeleza ahadi aliyoupa
Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Mjini hapo ofisini kwao
Miti ulaya Mjini Zanzibar.
Vifaa hivyo ambavyo ni Kompyuta
moja, Printa yake pamoja na Mashine ya Foto kopi vitasaidia pia
Jumuiya nyengine za CCM Ofisini hapo vikiwa na thamani ya shilingi
za Kitanzania Milioni Tatu na Laki Tano { 3500,000/- }.
Mama Asha akiwa pia na wadhifa wa
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini
“ B “ alisema wananchi wataelewa kazi hiyo kubwa iwapo Viongozi
wa CCM Ngazi mbali mbali watafanya juhudi za makusudi katika
kuyaeleza mafanikio hayo kwa Wananchi.
Alisema tabia ya kusubiri Viongozi
wa ngazi ya juu kuyaeleza mafanikio hayo na wale wengine wa ngazi za
kati wakijibweteka ni ya hatari na inaweza kudhoofisha nguvu za
Chama hicho.
Alifahamisha kwamba wananchi walio
wengi ndani ya Taifa hili wana imani na matarajio ya kukiona chama
cha Mapinduzi kinaendelea kuiongoza Tanzania kwa vile sera na ilani
yake ndio iliyopata ridhaa ya Umma.
“ Tunataka kuona Chama cha
Mapinduzi kinaendelea kuongoza Taifa hili katika muda wote “.
Alisema Mama Asha.
Alieleza kwamba kazi za Chama
hutekelezwa na wanachama wote wakisimamiwa na viongozi wao wa ngazi
zote.
Mama Asha aliwafahamisha Viongozi
hao wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa na Wilaya ya Mjini kwamba muda wote
atakuwa tayari kushirikiana nao katika kuona utekelezaji wa ilani ya
CCM na Sera zake unafanikiwa ipasavyo.
Alisema wakati umefika kwa viongozi
na wanachama wote wa Chama hicho kuwadharau watu na hata wale
viongozi wa upinzani wenye tabia ya kukejeli maendeleo yaliyofanywa
na CCM ambayo yako wazi.
Akitoa shukrani kwa niaba ya
viongozi wenzake Mwenyekiti wa Jumuiya Wazazi Mkoa wa Mjini Ndugu Ali
Othman Said alimpongeza Mama Asha kwa jitihada zake za kusaidia jamii
katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Nd. Othman alisema jitihada hizo
zimekuwa zikishuhudiwa na wananchi bila ya kujali itikadi za
kisiasa, Kidini na hata kijinsia.
Akimuhakikishia Mama Asha utumiaji
sahihi wa vifaa hivyo Mwenyekiti huyo wa Wazazi Mkoa Mjini alisema
Chama Wazazi Wilaya na hata mkoa kimepata nguvu za utekelezaji mzuri
wa majukumu yake kutokana na msaada huo.
Alielezea faraja yake na kusema
kwamba vifaa hivyo kwa kiasi kikubwa vitapunguza matumizi makubwa ya
fedha za Jumuiya hiyo ambapo kazi zake nyingi zilikuwa zikifanywa kwa
malipo katika maeneo ya nje jambo ambalo lilikuwa likiondosha usiri
wa kazi za Jumuiya hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
19/10/2014.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni