Ofisa Mkuu Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Peter Ngota (kushoto) akizungumza na wanahabari mara baada ya mkutano wa wadau wa mawasiliano Afrika ikiwemo kampuni ya TTCL. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
KAMPUNI ya Simu nchini Tanzania (TTCL) imeanzisha
kituo cha kuuzia huduma za interneti 'IP Pop -Internet Protocol Point of
Presence' nchini ikiwa ni jitihada za kuboresha huduma za mawasiliano
zaidi. Huduma kama hii awali ilikuwa ikinunuliwa nje hasa makampuni
anuai yanayotoa huduma hizo barani ulaya.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Mkuu Mauzo na Masoko
wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Peter Ngota alipokuwa akizungumza na
wanahabari katika mkutano wa wadau anuai wa mawasiliano kutoka nchi za
Afrika Mashariki na baadhi za mataifa ya Afrika unaofanyika Tanzania.
Ngota alisema kampuni ya TTCL imekuwa na mchango mkubwa wa kusimamia
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuwawezesha Watanzania na hata nchi
jirani kupata mawasiliano mazuri kutoka katika nchi zao hadi katika nchi
za ulaya.
"...Kuna juhudi mbalimbali TTCL
tunafanya ili kuongeza fursa kwenye mawasiliano ambapo kwa sasa
tumefungua kituo cha kuuzia interneti hapa nchini, kinaitwa IP Pop
(Internet Protocol Point of Presence). Awali interneti tulikuwa tunaenda
kununulia London kwenye makampuni mbalimbali sasa hivi tumeanzisha
kituo chetu cha kununulia intaneti hapa hapa nchini...Kwa hiyo
tunawakaribisha watumiaji wa interneti kuja kununua huduma hizi kwetu,"
alisema Ngota.
Akizungumzia mkutano huo, Ngota
alisema wadau wa mawasiliano Afrika ikiwemo TTCL imejipanga vizuri
kutumia fursa ambazo zinaweza kupatikana nchini na nje ya nchi ili
kuendeleza sekta ya mawasiliano. "...Unapopiga simu lazima uende hadi
nchi za nje kupata ile njia alafu ndo unarudi ulipo Afrika sasa hivi
tunaangalia namna gani tutajikwamua na huduma kama hizo kuzipata hapa
hapa Afrika..." alisema ofisa huyo wa TTCL.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba akizungumzia mkutano huo alisema mkutano huo ni muhimu kwani
wadau wa mawasiliano wamekutana kujadili maendeleo ya sekta ya
mawasiliano, hasa katika ukanda wa afrika mashariki na afrika kwa
ujumla. Alisema Tanzania inategemewa sana na nchi karibia saba ambazo
zipo pembezoni mwa bahari kupitia huduma ya mkongo wake wa mawasiliano.
"Mkongo
wa mawasiliano wa kimataifa umetua katika bahari yetu na sisi tunauza
huduma hiyo kwa nchi nyingine...Tumeupeleka hadi kwenye mipaka ya
majirani zetu kama Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia na wengineo ambao
hawana mawasiliano."
Makamba alisema mpango wa
Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata mawasiliano mazuri na
yalio bora maana hiyo ni haki yake. Sera na kanuni za Serikali ni
kuhakikisha hilo linafanikiwa. Aliongeza kuwa kwa kulitambua hilo
Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kujenga mkongo wa taifa wa
mawasiliano.
"..Na sasa tunaingia kwenye awamu
ya tatu ya upanuzi wa mkongo huo ikiwa ni sambamba na uboreshaji wa
mawasiliano, ili ufike kila wilaya nchini, Watanzania wengi maeneo ya
vijijini bado hawana mawasiliano, sehemu nyingine hakuna mawasiliano
kabisa au pengine yapo lakini si mazuri.
Aidha
alibainisha kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2015
maeneo yote ambayo hayana mawasiliano yanapata mawasiliano, hii ni
pamoja na kukaribisha makampuni mapya yaweze kuwekeza katika sekta hii
ili uwepo ushindani kwamba kama kuna maeneo kampuni fulani haitaki
kwenda basi nyingine ziende huko.
"...Mkongo wa
taifa wa mawasiliano ni biashara na majirani zetu wanategemea na
wananunua huduma hiyo kutoka kwetu. Tunachokifanya ni kuiimarisha
kampuni ya TTCL hadi sasa wanafanya kazi nzuri sana wana wadau na
washirika wengi toka nchi jirani ambapo wanafanya nao biashara. Kazi ya
Serikali ni kuiwezesha ili biashara hiyo iwe kubwa zaidi," alisema
Makamba.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni