Taarifa ya benki ya biashara ya
Mkombozi juu ya sakata la Escrow
Utangulizi
Taarifa hii inatolewa kwa umma kutokana na ripoti mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari mitandao ya kijamii na taarifa iliyotolewa kwenye mjadala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1. Ufunguzi wa akaunti ya VIP
engineering and Marketing (VIP)
Kampuni ya VIP engineering and
Marketing ni kampuni ambayo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za
Tanzania. Kampuni hii ilifungua akaunti katika benki ya biashara ya
Mkombozi na hivyo kuwa moja kati ya wateja wa benki. Benki
ilijiridhisha na ilizingatia taratibu zote za ufunguzi wa akaunti
husika kwa kuzingatia sheria za nchi na kanuni zinazozitaka benki
kupata nyaraka muhimu kutoka kwa mteja wakati wa ufunguzi wa akaunti
hiyo.
Nyaraka hizo ni pamoja na kuwepo kwa
cheti cha usajili wa kampuni, kanuni za kampuni, idhinisho la kampuni
kumruhusu moja kati ya wanahisa wake kuendesha akaunti pamoja na
picha na hati ya kusafiria ya mhusika wa kuendesha akaunti hiyo.
2.0 Mauzo ya hisa za VIP
Kampuni ya VIP ilileta mkataba
kwenye benki ya Mkombozi wa mauziano ya hisa za asilimia 30 baina ya
VIP na kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) ambazo inamiliki
katika kampuni ya IPTL. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 19 Ogasti,
2013. Bei ya asilimia 30 ya hisa hizo ilikuwa ni dola za Marekani
milioni 75. Katika kifungu namba 2.4 cha mkataba wao kinaelekeza
fedha za mauzo ya hisa zilipwe kwenye akaunti ya VIP iliyopo benki ya
Mkombozi. Mkataba huo wa mauziano ya hisa baina ya kampuni hizi mbili
ulitambuliwa na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa na
Jaji J.H.K Utamwa tarehe 5 Septemba, 2013.
3. Mchakato wa kulipa kodi ya
serikali
Benki ilitambua kwamba katika
mauziano hayo ya hisa ni lazima kodi ya Serikali ilipwe na hivyo
iliizishauri pande zote mbili kupeleka mkataba husika katika ofisi za
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanyiwa makadirio ya kodi
husika. Tarehe 20 Januari, 2014 TRA iliiandikia barua kampuni ya VIP
na nakala ya barua hiyo kuletwa kwenye benki ya Mkombozi. Katika
barua hiyo TRA iliitaarifu kampuni ya VIP kuwa makadirio ya kodi
yatokanayo na mauzo ya hisa ni shilingi 38,186,584,322.00 ikiwa ni
kodi ya mauzo ya hisa ya asilimia 30 za mauzo ya hisa kutoka VIP
kwenda kwa PAP.(Capital gains and stamp duty).
TRA pia iliiagiza benki ya Mkombozi
kuhakikisha kuwa inalipa kodi hiyo kwa niaba ya VIP mara tu fedha
zitakapoingia kwenye akaunti yake.
Malipo ya kodi ya shilingi
38,186,584,322.00 yalilipwa TRA kwenye akaunti 11120100 iliyopo
katika Benki Kuu ya Tanzania na TRA ilikiri kupokea kodi hiyo kwa
barua yake yenye kumbukumbu namba 3-4/100/100/223/4 ya tarehe 24
Januari, 2014.
4. Ufafanuzi wa mambo mbalimbali
4.1 Benki ya mkombozi kuhusika
katika kusafisha fedha chafu
Fedha zote zilizoingizwa kwenye
akaunti ya VIP iliyopo kwenye benki ya Mkombozi zilitokana na
mauziano ya hisa kati ya VIP na PAP kwa mkataba uliotambuliwa na
Mahakama Kuu ya Tanzania. Chanzo cha malipo hayo ni kuhamisha fedha
kutoka kwenye akaunti ya PAP iliyopo katika benki ya Stanbic na
kuingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo katika benki ya Mkombozi.
Fedha hizo zilihamishwa katika
mafungu mawili. Fungu la kwanza ilikuwa ni shilingi 73,573,500,000.00
zilihamishwa kwa njia ya TISS kwa kumbukumbu namba 000000050720 ya
tarehe 23 Januari, 2014 na fungu la pili ni dola za Kimarekani
22,000,000.00 zilihamishwa kwa TISS kwa kumbukumbu namba000000050812
ya tarehe 23 Januari, 2014. Malipo mengine ya asilimia kumi ya mauzo
ya hisa yalilipwa kwenye akaunti ya Mkombozi iliyopo Benki Kuu ya
Tanzania. Kutokana na mchakato huo benki ya Mkombozi ilijiridhisha
kuwa fedha hizo ni malipo halali na siyo fedha chafu.
Benki ya Mkombozi haijihusishi na
utakasishaji wa fedha chafu na haramu katika uchumi wa Tanzania.
4.2 Malipo yatokanayo na akaunti ya
VIP
Malipo toka kwenye akaunti ya mteja
hufanywa kutokana na maelekezo ya mteja. Benki ikishajiridhisha kuwa
fedha ya mteja ni halali na ipo kwa mujibu wa sheria na hamna zuio
lolote toka katika mahakama hapa nchini hutekeleza malipo kwenye
akaunti ya mteja kutokana na maelekezo yake.
Benki ilijiridhisha kuwa malipo yote
yaliyofanywa kutoka kwenye akaunti ya VIP ni halali kwa kuwa chanzo
cha pesa hizo ilikuwa ni halali kutokana na mauzo ya hisa na ulipwaji
wa kodi ya Serikali kama ilinyoelezwa hapo juu. Kutokana na sababu
hiyo benki haikuwa na shaka juu ya malipo hayo.
4.3 Malipo taslimu kwa wateja na
kubeba fedha kwenye viroba, mifuko ya rambo na magunia
Benki inatoa tamko kuwa malipo yote
yaliyofanywa katika akaunti ya VIP yalilipwa kupitia akaunti za
walipwaji. Hakuna fedha zilizolipwa taslimu kwa wateja na kubebwa
kwenye viroba au magunia kama ilivyoripotiwa Bungeni. Pesa iliyotoka
kwenye akaunti ya VIP tarehe 6 Februari, 2014 kiasi cha shilingi
3,314,850,000.00 ililipwa kwenye akaunti nane za wateja tofauti na
siyo kubebwa kwenye viroba au magunia.
Na zile zilizotoka toka benki ya
Stanbic zilizotajwa hapo juu zilitumwa kwa njia ya TISS na siyo
kubeba kwenye magunia au viroba.
4.4 Malipo kwa mfanyakazi wa benki
ya Mkombozi
Gazeti la Mawio la tarehe 20-26,
Novemba, 2014 tolea namba 0122 liliandika kuwa mwanasheria wa benki
ya Mkombozi ajulikanaye kwa jina la Rweyengeza Alfred alipokea malipo
toka akaunti ya VIP ya shilingi milioni 40.2.
Benki inatoa tamko kuwa haina
mfanyakazi anayetambuliwa kwa jina hilo na wala hakuna mfanyakazi
yeyote wa benki aliyelipwa fedha toka kwenye akaunti ya VIP.
Wito kwa umma
Benki ya Mkombozi inachukua fursa
hii kuwatarifu wateja wake na umma kutopotoshwa na taarifa au tuhumma
zilizofafanuliwa hapo juu na kuwataka wateja wake wote kutokuwa na
hofu yeyote kwani benki ipo imara na inafanya kazi kwa kufuata
misingi ya sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na Benki Kuu ya
Tanzania. Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla
kutoyumbishwa na tuhumma hizo ambazo hazina ukweli ndani yake na
badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi
yetu.
Pamoja tunajenga nchi na uchumi wa
nchi yetu.
Hitimisho
Benki ya biashara ya Mkombozi
haijihusishi na haitajihusisha na utakasishaji wa fedha chafu.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MTENDAJI BENKI YA
BIASHARA YA MKOMBOZI

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni