Na Anna Nkinda – Lindi
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
amewataka wakazi wa Kata ya Ng’apa wilaya ya Lindi mjini kuchagua
viongozi waadilifu na wenye sifa ambao watawaongoza wananchi
kusimamia shughuli za maendeleo yao.
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia
wilaya ya Lindi mjini alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na
wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa Wenyeviti na
Wajumbe wa Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata hiyo.
Mama Kikwete alisema kuna baadhi ya
watu wanachagua viongozi kwa ushabiki pasipo kuangalia kiongozi huyo
kama ana sifa au la, na kuwasisitiza wananchi hao siku ya uchaguzi
ikifika wasifuate mambo ya ushabiki na kuchagua kiongozi kwani
ushabiki hauna manufaa yoyote.
“Nawaombeni muwapigie kura za
ndiyo viongozi wote wa CCM wanaogombea nafasi za Wenyeviti na
Wajumbe wa Serikali za Mitaa, kwani hawa wanasifa na mkiwachagua
kutakuwa na manufaa kwenu na vizazi vyenu hivyo basi wote
mliojiandikisha siku ya uchaguzi ikifika mjitokeze kupiga kura na
kukichagua Chama chetu”, alisema .
Aidha MNEC huyo aliwakumbusha
wanachama wa CCM siku ya uchaguzi kutokwenda kupiga kura wakiwa
wamevaa sare za Chama au mavazi yoyote yenye kuonyesha ushabiki wa
Chama cha siasa hiyo hairuhusiwi na kwa kufanya hivyo ni kwenda
kinyume na Maadili ya vyama vya Siasa na Sheria ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi .
Kuhusu elimu Mama Kikwete alisema
Serikali ya CCM kwa kushirikiana na wananchi imefanikiwa kujenga
shule za Sekondari nchi nzima na ifikapo mwakani maabara kwa ajili
ya masomo ya sayansi katika shule hizo zitakuwa zimekamilika na
kuanza kutumika.
Alisema, “Ninawaomba wazazi na
walezi msimamie watoto waende shule ili wawe na maisha bora hapo
baadaye kwani tatizo kubwa lililoko hapa ni watoto kutokwenda shule.
Serikali imewajengea shule na maabara lakini kama watoto wenu
hawataenda shule ni kazi bure, ili shule hizi ziwe na faida kwenu ni
lazima watoto wenu wasome”.
Mama Kikwete pia alitembelea Kata ya
Makonde na kuongea na wanachama pamoja na wagombea wa nafasi za
Uenyeviti na Wajumbe na kuwapongeza viongozi wa zamani ambao
wanamaliza kipindi chao cha uongozi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya
kutekeleza na kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Aliwapongeza wanawake waliojitokeza
na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi jambo ambalo litawawezesha
kuingia katika ngazi ya maamuzi.
Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa
ajili ya shughuli za kichama ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye
kampeni na kuwanadi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi
mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za
Mitaa, Vijiji na Vitongoji utakaofanyika tarehe 14 mwezi huu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni