Katibu wa Kamati ya Bandari ya
Nyanjale Kiomba Mvua Bwana Moh’d Ali akitia saini makubaliano
yaliyofikiwa baina ya Wanakijiji hicho na Uongozi wa Hoteli ya
Kimataifa ya Sea Cliff iliyopo Kama nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Waliosimamanyuma yake wakishuhudia tukio hilo kutoka kulia ni
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Haji Juma Haji, Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja Kana Mstaafu Juma Kassim Tindwa, Mwakilishi wa Jimbo
la Kitope Mh. Makame Mshimba Mbarouk, Mwanasheria wa Makamu wa Pili
Bibi Mwanaisha Shamte,Menaja Mkuu wa Sea Cliff Bwana Abre Esterhuizen
na Mwanasheria wa Wizara ya Ardhi Nd, Khamis Faraji.
Wajumbe wawili wa Kamati ya Bandari
ya Kiomba Mvua Bwana Othman Ashkina na Bibi Chiku Sheikh wakimwaga
wino kwenye maridhiano waliyofikia na Hoteli ya Sea Cliff.Wajumbe hao
wanashuhudiwa nyuma na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kanal
Mstaafu Juma Kassim Tindwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Haji
Juma Haji na Afisa Tawala Wil;aya ya Kaskazini B Nd. Juma Abdulla.
NI Sheha wa Shehia ya Kiomba Mvua
Bwana Mzee Ramadhan Mzee akitia saini kama shahidi Makubaliano ya
maridhiano kati ya Wananchi wa Kiomba Mvua na Uongozi wa Hoteli ya
Sea Cliff.
Zamu ya Meneja Mkuu wa Hoteli ya Sea
Cliff Bwana Abre Esterhuizen akimwaga wino kwenye maridhiano hayo ya
makubaliano na wana Kijiji cha Kiomba Mvua.
Menaja Utawala na Uendeshaji wa
Hoteli ya Sea Cliff Bwana Abdulmalik Mussa Kushoto na Meneja wa
Mchezo wa Golf wa Hoteli hiyo Bwana Heirz Papenfus wakijumuika kutia
saini Mkataba huop wa maridhiano.
Balozi Seif akishuhudiwa na Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Unguja Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa Kulia yake
na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo kushoto yake Nd. Haji Juma Haji
chini ya usimamizi wa Mwanasheria wa Makamu wa Pili aliyesimama Bibi
Mwanaisha Shamte akitia saini kama shahidi kwenye mkataba wa
maridhiano hayo.
Balozi Seif akimpongeza Katibu wa
Kamati ya Bandari ya Nyanjale Kiomba Mvua Bwana Moh’d Ali mara
baada ya kumalizika kwa zoezi la utiaji saini mkataba wa maridhiano
kati ya Uongozi wa Hoteli ya Sea Cliff na Wana Kijiji wa Kiomba Mvua.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR –
ZNZ.
Press Release:-
Hatma njema ya Kikao Maalum
kilichotayarishwa kwa ajili ya utiaji saini makubaliano baina ya
Muwekezaji wa Hoteli ya Kimataifa ya Sea Cliff iliyopo katika Kijiji
cha Kama na Wananchi wanayoizunguuka Hoteli hiyo imefikiwa.
Utiaji saini makubaliano hayo
ulikuwa ufanyike Tarehe 10 Mwezi Mei Mwaka huu lakini ulishindikana
baada ya uamuzi wa wajumbe wa upande wa Kamati ya Bandari ya Nyanjale
Kiomba Mvua kutokufika katika kikao hicho bila ya sababu
zisizoeleweka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja, Taasisi za Ardhi na Mazingira walishuhudia utiaji
saini huo ambapo upande wa Hoteli ya Sea Cliff uliwakilishwa na
Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo Bwana Abre Esterhuizen,Meneja wa Mradi wa
Mchezo wa Golf wa Hoteli hiyo Bwana Heirz Papenfus pamoja na Meneja
Utawala na Uendeshaji wa Hoteli Bwana Abdullmalik Mussa.
Upande wa wana kijiji cha Kiomba
Mvua ukaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bandari ya eneo hilo Nd.
Mbwana Amour Khamis, Katibu wa Kamati hiyo Nd. Moh’d Ali Ameir
pamoja na wajumbe wawili Bibi Chiku Sheikh Nd. Othman Ashkina.
Hafla hiyo ya utiaji saini Mkataba
huo wa makubaliano ilifanyika katika ukumbi wa Hoteli hiyo ya
Kimataifa ya Sea Cliff iliyopo Kama kilomita chache kaskazini ya Mji
wa Zanzibar.
Mgogoro baina ya Muwekezaji huyo na
Wananchi wa Vijiji jirani ambao ulihusu zaidi eneo la Bandari ya
Madagaa pamoja na bara bara iendayo eneo hilo ulifikia makubaliano
kufuatia vikao mbali mbali vilivyokuwa vikiendelea katika kutafuta
maridhiano ya pande zote mbili.
Vikao vya pamoja kati ya Uongozi wa
Hoteli ya Sea Cliff na Viongozi wa Kamati Nne za Vijiji vya Kiomba
mvua vilikuwa vikifanyika kwa pamoja kupitia muongozo ulitolewa na
Kamati ya Baraza la Wawakilishi kuhusu maridhiano ya pande hizo
husika.
Mazingira halisi ya mgogoro wa
Kiomba mvua na Muwekezaji wa Sea Cliff umefikia hatua nzuri ya
maridhiano lakini kilichokuwa kikionekana wakati wa kufikia hatma
yake ya mwisho ni baadhi ya watu kuanza kuhusisha mgogoro huo na
masuala ya Kisiasa.
Akizungumza kwenye Kikao hicho
Mwakilishi wa Mradi wa Hoteli ya Sea Cliff Bwana Yassir De Costa
ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
jitihada zake inazochukuwa katika kuunga mkono Taasisi za uwekezaji
vitega uchumi hapa nchini.
De Costa alisema katika muelekeo wa
kusaidia maendeleo ya wananchi wa vijiji vya jirani, Mradi wa Hoteli
ya Sea Cliff umeamua kusaidia utunzaji wa mazingira ya Mikoko,
kuwapatia Gari ya usafiri, kujenga mabanda ya wavuvi na vyoo vyake
pamoja na ujenzi wa bara bara.
Alisema huduma hizo zitakwenda
sambamba na wananchi hao kupatiwa Eka moja na nusu kwa ajili ya
uanikaji wa dagaa, fedha taslim shilingi Milioni 11 zitakazohudumia
bidhaa zao kuhamia eneo jipya pamoja na shilingi milionji 16 kwa
ajili ya kuendeleza kamati hiyo.
Alieleza kwamba wakaazi wote
wanaozunguuka mradi huo watakuwa na fursa ya kupatiwa huduma za Afya
katika Kituo cha Afya cha Hoteli hiyo ambapo utaratibu utaandaliwa
kwa mgonjwa atakayezidiwa maradhi kwa kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya
Mnazi Mmoja.
Akitoa nasaha zake mara baada ya
zoezi hilo la utiaji saini makubaliano hayo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza wananchi wa kiomba mvua
kwa uamuzi wao huo na kuwataka waendelee kushirikiana na wawekezaji
ili kusaidia kuimarisha uchumi wa taifa kupitia sekta ya uwekezaji.
Balozi Seif ambae pia ni Mbunge wa
Jimbo la Kitope linalounda eneo hilo alisema Viongozi Wakuu wa
Serikali wamekuwa wakisafiri nchi tofauti kujaribu kubembeleza
wawekezaji wan chi hizo kuja kuwekeza miradi yao nchini ili kusaidia
kunyanyua uchumi wa Taifa.
Hata hivyo Balozi Seif alionyesha
masikitiko yake kutokana na kitendo cha kutiwa saini makubaliano hayo
kuchelewa kwa karibu mwaka mzima kutokana na sababu za tatizo hilo
kuingizwa siasa jambo ambalo linavuruga maendeleo ya jamii.
“ Mara nyingi nimekuwa nikialikwa
kuzindua miradi ya wananchi katika Mkoa wa Kusini Unguja
inayogharamiwa na wawekezaji. Hivyo ni vyema kwa wanakijiji cha
Kiomba mvua na vijiji vyengine nchini wakaiga mfano huo wa wenzao wa
Mkoa wa Kusini “. Alisema Balozi Seif.
Aliwaomba wananchi hao kuhakikisha
kwamba yanapojitokeza matatizo baina yao na Taasisi au Makampuni
yanayowekeza katika maeneo yao kwenda katika ngazi zinazohusika
badala ya kukimbilia kupatuka kwenye vyombo vya Habari.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini
Unguja Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa alisema Taifa bado linaendelea
kukabiliwa na tatizo la umaskini ambapo muhimili wa kusaidia mapato
ya Nchi kwa sasa ni kukaribisha Makampuni na Taasisi katika sekta ya
uwekezaji.
Kanal Mstaafu Tindwa alifahamisha
kwamba Sekta ya uwekezaji hasa katika miradi ya Utalii Nchini hivi
sasa imekuwa ikisaidia kwa kiwango kikubwa miraji ya Kiuchumi,kijamii
kwa asilimia pana zaidi.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Kaskazini
Unguja aliiagiza Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa huo kuhakikisha
kwamba inadhibiti na kuchukuwa hatua za kisheria kwa mtu au kikundi
chochote kinachojaribu kuvuruga miradi ya uwekezaji na maendeleo ya
wananchi katika Mkoa huo.
Mhe. Tindwa alikemea tabia ya
baadhi ya watu walioamua kuiba tangi la kuhifadhia maji na baadhi ya
milango kwenye soko lililojengwa na Hoteli ya Sea Cliff kwa ajili ya
wananchi na wavuvi hao wa Kijji cha Kiomba Mvua.
Akitoa shukrani kwa niaba ya
wananchi na wavuvi wenzake wa Kijiji cha Kiomba Mvua Katibu wa Kamati
ya Bandari ya Kijiji hicho Bwana Mbwana Moh’d Ali Ameir alisema
wananchi hao watakuwa tayari kushirikiana na uongozi wa mradi huo ili
malengo yaliyokusudiwa yafikiwe.
Katibu Moh’d akiomba radhi
kutokana na matokeo yaliyojitokeza kwenye mgogoro huo alisema moja
kati ya jukumu walilokubali kulibeba wana kjijiji hao ni kuhakikisha
suala la mazingira ya eneo hilo linalindwa na kuwa katika hali ya
kuridhisha.
Mgogoro baina ya muwekezaji wa
Hoteli ya Sea Cliff na wanakijiji wanaoizunguuka Hoteli hiyo ulikuwa
ukivukuta katika suala la matumizi ya bandari, eneo la kuanikia
madagaa pamoja na bara bara mambo ambayo muwekezaji huyo ameyakubali
kuyatekeleza kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
4/12/2014.







Hakuna maoni :
Chapisha Maoni