.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 28 Februari 2015

SERIKALI KUFUFUA BANDARI 14 ZIWA NYASA – WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Mizengo amesema Serikali imeamua kufufua bandari ndogo 14
kwenye mikoa mitatu inayozunguka Ziwa Nyasa ili kuimarisha usafiri wa majini kwa wakazi wa Ruvuma, Njombe na Mbeya.

“Tangu mwaka 2006 bandari za kwenye mikoa ya Ruvuma, Njombe na Mbeya
zilikufa na hivyo kuleta shida ya usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo lakini Serikali imeamua kuzifufua bandari hizo na Itungi itakuwa ndiyo kituo kikuu cha bandari zote katika Ziwa Nyasa,” alisema Waziri Mkuu.

Alikuwa akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Kyela kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika jana jioni (Jumatano, Februari 26, 2015) kwenye uwanja wa michezo wa Mwakangale na kuhudhuriwa na maelfu ya wakazi wa
wilaya hiyo.

Alizitaja bandari hizo kuwa ni Ndumbi, Lundu, Njambe, Mkili, Liuli, na Mbamba bay ambazo ziko mkoani Ruvuma. Nyingine ni Lumbila, Ifungu, Nsisi, Lupingu na Manda ambazo ziko Njombe wakati bandari za Mbeya ni Itungi, Kiwira na Matema.

Alisema ili kufanikisha hilo, Serikali imehamisha chelezo (Dry Dock) kutoka bandari ya Mwanza na kwamba mkandarasi kutoka Kampuni ya Songoro Marines, ameshaanza ujenzi wa chelezo hiyo.

“Baada ya kukamilika, Chelezo hiyo, itatumika kutengenezea meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo na kufanya ukarabati wa meli pindi zinapohitaji matengenezo. Nimeambiwa na mkandarasi kutaka watamaliza hii kazi ifikapo Juni, mwaka huu,” alisema huku akishangiliwa na umati huo.

Waziri Mkuu alisema, mbali ya hilo, chelezo hiyo pia itatumika kutengeneza matishari mawili ya kubebea mizigo ambayo yatakuwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 1,000 kila moja.

“Yatatumika kusafirisha mizigo hiyo hususan mazao ya wakulima kupitia
bandari ndogo zilizopo lakini pia yatasafirisha tani 60,000 za makaa ya mawe, tani 72,000 za saruji kutoka Mbeya kwenda Malawi na mikoa jirani; tani 10,000 za mbolea kutoka Dar es Salaam pamoja na chuma kutoka Liganga na Mchuchuma,” alisema.

“Chelezo hiki kitakapokamilika kitakuwa kikubwa na cha aina yake…hakuna kingine cha kulinganishwa nacho katika nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji. Itumieni fursa hii kwa kutunza ule mto kwenye mdomo wa kuingilia bandari ya Itungi, msilime kwenye kingo za mto,” aliongeza.

Mapema, akizungumza na wakazi wa kata ya Lusungo mara baada ya kuweka
jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Lusungo, Waziri Mkuu Pinda alisema daraja hilo ni kiungo muhimu kwenye barabara hiyo iendayo kwenye bandari ya Matema.

Aliwataka wakazi wa kata hiyo walitunze daraja hilo ili liweze kuwasaidia kusafirisha bidhaa na mazao wanayolima. Ujenzi wa daraja hilo, ambalo limejengwa kupitia mfuko wa barabara, lina urefu wa mita 50 na upana wa mita 7.3 pamoja barabara yenye urefu wa mita 600 kutoka kwenye maingilio ya daraja hilo, limegharimu kiasi cha sh. bilioni 3.7 huku ujenzi wake ukiwa umekamilika kwa asilimia 99.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda alipewa jina la MWAKABULUFU
na Chifu Ernest Mwailemale wakati akisimikwa kuwa kiongozi wa eneo hilo la Lusungo. Waziri Mkuu alivishwa mgolole na kupewa mkuki ili autumie kuilinda nchi dhidi ya maadui kutoka pande zote.

Akizungumza mara baada ya kumsimika Waziri Mkuu, Chifu Mwailemale
mwenye umri wa miaka 91, alisema jina hilo ni la babu yake mzaa baba
ambaye aliwahi kutawala eneo hilo. Hata hivyo, hakutaja ni mwaka gani.

Alipoulizwa maana ya jina hilo, Chifu Mwailemale ambaye wakati wote alikuwa akizungumza Kiswahili kwa ufasaha alisema: “Jina hili halina maana maalum bali na heshima kwa sababu lilikuwa la Chifu aliyetawala eneo hili,” alisema na kufafanua kuhusu umri wake: “Nina miaka 91 kwa maana nilizaliwa tarehe 25 Septemba mwaka 1924,” alisema Chifu huyo ambaye anaelezwa kupigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni