.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 31 Machi 2015

BALOZI SEIF AWATAKA WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO VYEMA


                                                                                    Picha na – OMPR – ZNZ.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wanaposhughulikia mambo ya Kitaifa kuweka kando jazba zao na badala yake kutekeleza vyema wajibu unaowahusu kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Nchi ili lile wanalotarajia kuwafikia wananchi liweze kupatikana.

Alisema ni vyema Wawakilishi hao wakawa na hadhari na wanayoyajadili na kuelewa kwamba Wananchi walio wengi wanafuatilia matendo yao ndani ya Baraza la Wawakilishi na iko siku wananchi hao watafikia uwamuzi wa kuwahukumu kwa matendo yao.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akiufunga Mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukiendelea katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema mambo yaliyotokea ndani ya Baraza hilo Tarehe 11Machi mwaka huu wakati wa kuwasilishwa sheria ya Kura ya Maoni nambari 11 ya mwaka 2013 ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Kifungu 131 (2) cha Katiba ya Zanzibar mwaka 1984 yamewasikitisha Wananchi walio wengi.

Alisema yaliyotokea ndani ya Baraza hilo ambayo yalifanywa na baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo hayakuwasilisha vizuri Baraza hilo mbele ya macho ya Wananchi wanaowawakilisha katika Chombo hicho muhimu kikiwa miongoni mwa mihimili mitatu ya Nchi hii.

Balozi Seif alifahamisha kwamba kupitia vyombo mbali mbali vya Habari vilivyokuwa vikurusha matangazo ya muendelezo wa Vikao vya Baraza hilo Wanachi wengi wameshuhudia mchezo wa baadhi ya wawakilishi hao badala ya kufanya kazi waliyotumwa.

Alitahadharisha kwamba kuhitilafiana kwenye Baraza au bunge wakati wa mijadala ya waheshimiwa ni mambo ya kawaida, lakini itapendeza kuona kuwa busara inatumika katika jambo wanalotofautiana waheshimiwa hao badala ya jazba.

Aliwaomba Viongozi wote wa Kisiasa na wa Kijamii pamoja na Wananchi kushirikiana na Serikali katika kuendeleza na kudumisha amani na utulivu uliopo katika Taifa hili.

Akitoa ufafanuzi wa suala la vitambulisho vya Mzanzibari ambalo lilionekana kuibua mjadala mkali ndani ya baraza hilo na kutishia utulivu wa mijadala ya wawakilishi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kila Mzanzibar anastahiki kupata kitambulisho hicho baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa kisheria.

Balozi Seif aliwanasihi waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuepuka jazba na utashi wa kisiasa wakati wanapojadili hoja mbali mbali wakielewa kwamba masuala mengine ni ya kisheria, sheria ambazo wamezitunga wao wenyewe.

Alisisitiza na kuwaomba Waheshimiwa pamoja na Wananchi kuelewa kuwa Serikali kamwe haitamnyima haki Mzanzibari ye yote aliyetimiza masharti ya kupata Kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi.

Alifahamisha kwamba ni wajibu wa Waheshimiwa na Viongozi wote kuendelea kuwaelimisha Wananchi juu ya utaratibu wa kisheria uliopo na kuwataka kuufuata utaratibu huo bila ya kuweka shindikizo za kisiasa.

Akizungumzia matumizi bora ya ardhi Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali imekamilisha Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya Ardhi wa Zanzibar ambapo utekelezaji wake utasaidia kupunguza matumizi holela ya ardhi.

Alisema utayarishwaji wa sheria ya kuanzisha Kamisheni ya ardhi itakayosimamia matumizi yote ya ardhi nchini sambamba na kuimarishwa kwa Mahkama za Ardhi kwa kuzipatia vitendea kazi na kuziongezea idadi ya Mahakimu umelenga kupunguza tatizo la migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu hivi sasa.



Akigusia huduma bora za maji safi na Salama Balozi Seif alisema Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo bado inaendeleza jitihada zake za kuwatia Wananchi huduma hiyo muhimu ili kutimiza azma yake ya kusambaza huduma hizo mijini na Vijijini.

Alisema hatua maalum zimechukuliwa kwa kuziondoa mita 41 za Tukuza zilizokuwa zimefungwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } katika Visima mbali mbali vya miradi ya maji ili kuwaondoshea kero wananchi na kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama bila ya usumbufu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwanasihi wananchi wenye tabia ya kujenga katika vianzio vya maji kuacha mara moja hulka hiyoambayo inaweza kuhatarisha maisha na afya za wananchi wanaotumia huduma ya maji yenye kupatikana katika vianzio hivyo.

Kuhusu kura ya Maoni kwa Katiba inayopendekezwa Balozi Seif alisema ili kuhakikisha Watanzania wanafanya maamuzi sahihi ifikapo siku ya kupiga kura ya maoni, aliwaomba Wananchi kuisoma na kuielewa vyema Katiba inayopendekezwa.

Alisema maamuzi ya Wananchi hao ni vizuri yatokane na matakwa na ridhaa zao binafsi na sio kushawishiwa na watu, vikundi au vyama vya kisiasa kwa lengo la kupata Katiba itakayoliongoza Taifa la Tanzania katika kipindi chengine cha miaka 50 ijayo.

Alielezea matumaini yake kwamba Watanzania wote wataitumia fursa hiyo adhimu na adimu katika kuhakikisha Taifa lao linapata Katiba kwa kwenda kuipigia kura ya maoni Katiba inayoepndekezwa katika misingi ya amani, utulivu na usalama.

Akielezea masikitiko yake kutokana na Tanzania kukumbwa na wimbi la utekaji na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi { Albino } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalaani kwa nguvu zote vitendo hivyo.

Alisema Serikali pamoja na Wananchi wote wa Zanzibar wako pamoja na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua inazoendelea kuchukuwa katika kukabiliana na tatizo hilo.

Balozi Seif alitoa wito maalum kwa Wananchi wote kuongeza mapenzi na huruma baina yao katika kuwalinda na kuwathamini wananchi wenzao wenye ulemavu wa ngozi.

Mkutano huo wa 19 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar umejadili na kupitisha miswaada minne ya sheria ambayo ni Mswada wa sheria ya kuweka masharti ya usajili na usimamizi wa Wathamini na Mambo mengine yanayohusiana na hayo pamoja na Mswada wa sheria ya kuanzisha Kamisheni ya Ardhi na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mengine ni Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria nambari 6 ya Mwaka 1983 ya Baraza la Sanaa na Muziki na Sheria ya Bodi ya Sensa ya Filam na Utamaduni Zanzibar na mambo mengine yanayohusiana na hayo na ule Mswada wa sheria ya kufuta Sheria ya Miradi ya maridhiano nambari 1 ya Mwaka 1999 na kutunga sheria mpya kwa ajili ya kuanzishwa na kuendesha mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi na Mambo mengina yanayohusiana na hayo.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 13 mwezi Mei Mwaka 2015 mnamo saa 3.00 asubuhi.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni