Na Mwandishi Wetu
ASASI
ya Harakati za Imetosha ilioanzishwa kupinga mauaji na vitendo vya
kikatili wanavyofanyiwa watu wenye u-albino inatarajiwa kufanya
matembezi makubwa ya hisani kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendelea
kutoa elimu kwa uma juu ya imani potofu zinazoendelea za mauaji ya
albino.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo
jijini Dar es Salaam na Balozi wa Kujitolea wa Harakati za 'Imetosha
Movement', Henry Mdimu amesema matembezi ya hisani kuchangia fedha
zitakazowezesha kutolewa kwa elimu kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa juu ya
imani potofu zinazoendelea na mauaji ya albino yanatarajia kufanyika Dar
es Salaam Machi 28, 2015.
Alisema matembezi
hayo yataanzia katika Viwanja vya Leaders na kuzunguka maeneo
yaliyopangwa kisha kurejea viwanjani hapo kwa ajili ya shughuli maalumu
ya kuchangisha fedha kwa ajili ya harakati maalumu za imetosha zitakazo
kwenda kwa jamii ya kawaida na kueneza elimu ikiwa ni juhudi za
kuhamasisha kila mwana jamii kupaza sauti na kusema 'Imetosha Mauaji ya
Albino'.
"...Baada ya taratibu kukamilika,
matembezi sasa yatafanyika Tarehe 28 Machi kuanzia saa 12 Alfajiri,
kutoka Leaders Club tutazunguka na kurudi hapo, karibuni sana tuchangie
harakati hizi zenye lengo zuri kwa mustakabali wa Taifa letu lenye sifa
ya amani na utulivu," alisema Mdimu katika taarifa yake.
Aidha
akizungumzia uvumi ulioenea hasa katika nchi za nje, unaodai kwamba
serikali imekataza watu wenye ulemavu wa ngozi kuandaa matembezi au
maandamano alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote na kuongeza kuwa
kuna taratibu za kufuata kabla ya uandaliwa shughuli hizo.
"...Hili
suala sio kweli, ili ufanye mambo kama haya ni lazima upitie taratibu
za kisheria ili upate kibali. Hii ni nchi na ina taratibu zake kwa hiyo
tulipaswa kuzifuata na ndio kilichosababisha hata matembezi yetu
kuahirishwa.
"Tulikuwa tunafuata taratibu na
leo rasmi tumepata usajili wa Imetosha...sasa imetosha imekuwa taasisi
kamili inayoitwa IMETOSHA MOVEMENT. Napenda kuchukua wasaa huu
kuwashukuru marafiki wote wanaoniunga mkono, na kunipa moyo, msinichoke
kwa sababu safari bado ni ndefu,"
Hata hivyo
aliwataka wananchi na wadau mbalimbali yakiwemo makampuni kujitokeza
katika matembezi hayo ya hisani ili kuunga mkono juhudi sa mapambano ya
kukomesha mauaji na vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa watu wenye
ualbino maeneo mbalimbali ya nchi.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni