Zaidi ya wanafunzi 100 wa Chuo Kikuu
cha Nairobi nchini Kenya wamejeruhiwa leo alfajiri kwa kukanyagana
baada ya trasfoma ya umeme kulipuka na kuibua hali ya taharuki.
Tukio hilo lililotokea majira ya saa
kumi alfajiri limetokea katika kampasi ya Kikuyu, na kuibua hofu na
hali ya taharuki baada ya wanafunzi wengi kudhani mlipuko huo ni
tukio la kigaidi.
Hali hiyo ilipelekea wanafunzi hao
kuruka kutoka juu ya ghorofa wengine hadi kutokea ghorofa ya sita ya
hosteli yao katika kujaribu kujinusuru, ambapo wengi wao wamejeruhiwa
vibaya.
Wanafunzi wapatao 100, wamelazwa
katika hospitali ya Taifa ya Kenyatta, na wengine wamepelekwa
hospitali za Mtakatifu Teresa na Karen.
Tukio hilo limetokea baada ya wiki
mbili kupita tangu wanafunzi 148, kuuwawa katika Chuo Kikuu cha
Garissa kwa shambulio lililofanywa na magaidi wa kundi la Somalia la
al-Shabaab.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni