Na Mwandishi Wetu, Nangurukuru
KAMPUNI ya
Pan African Energy Tanzania Ltd imekabidhi msaada wa jengo lenye nyumba
mbili za wahudumu wa afya wa Zahanati ya Nangurukuru ikiwa ni jitihada
za kuisaidia Serikali kupunguza vifo vya akinamama na watoto katika eneo
la Nangurukulu na vijiji vya jirani.
Akikabidhi
majengo hayo jana kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Meneja Uwajibikaji kwa
Jamii wa Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd, Andrew Kashangaki
alisema lengo kubwa la misaada wanayotoa ni kuchangia maendeleo ya
kiuchumi na kijamii katika wilaya ambazo wanafanyia kazi zao.
Alisema
kuwa madhumuni ya msaada wa ujenzi wa nyumba hizo mbili waliozijenga
kwenye Zahanati ya Nangurukuru ni kuimarisha mahusiano mazuri na jamii
inayowazunguka maeneo ambayo wanafanyia shughuli zao.
Aidha
Kashangaki alisema mradi huo wa ujenzi wa nyumba za waganga umegharimu
zaidi ya milioni 458 za fedha za Kitanzania na zimejengwa kisasa ambapo
zinauwezo wa kubeba familia nne za watumishi wa Zahanati ya Nangurukuru
hali ambayo itasaidia.
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya ya Kilwa, Abdulah H. Ulega akipokea nyumba hizo alisema msaada
huo utapunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya akinamama wajawazito na
watoto eneo hilo ambapo awali vilikuwa vinatokana na huduma za afya kuwa
mbali na makazi ya akinamama hao.
"...Ni kweli
kwamba bado tunatatizo kubwa la vifo vya akinamama na watoto eneo letu
na vifo hivi vinachangiwa na tatizo la kukosekana kwa huduma za afya
karibu...kama inavyoeleza sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kusogeza
huduma za kijamii karibu na wananchi.
Aliongeza
kuwa Wilaya ya Kilwa kwa sasa inajitahidi kuhakikisha suala hilo
lakuendelea na ujenzi wa zahanati zaidi unafanya vizuri. "...Na moja ya
mafanikio yetu ni ujenzi wa Zahanati ya Nangurukuru na nyingine tano
tunazijenga, awali ilikuwa kati ya Vijiji 90 vya Wilaya yetu vilivyokuwa
na huduma za afya vilikuwa 43, lakini ndani ya miaka mitatu
tumejitahidi kuunga mkono juhudi za wanakijiji walipoanza mchakato wa
ujenzi wa zahanati kwenye vijiji vyao," alisema Mkuu wa Wilaya.
Kwa
upande wao baadhi ya wakazi waliohojiwa katika hafla hiyo ya
makabidhiano walisema ujenzi wa nyumba ya watumishi wa zahanati ya
Nangurukuru utawasaidia sana kihuduma za afya eneo hilo kwani awali
wananchi walikuwa wakilala barabarani wakati mwingine usiku wakisafiri
kutafuta huduma za afya.
Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Dodomezi, Mwanahawa Hamis alisema uzinduzi wa jengo la
zahanati hiyo utawasaidia hasa akinamama ambao walikuwa wanapoteza
maisha njiani kutokana na kutembea umbali kufuatilia huduma za afya.
Naye
Mwanawetu Mshamu Mkazi wa Kitongoji cha Dodomezi, mbali na kukabidhiwa
jengo la makazi ya watumishi wa afya aliiomba Serikali isaidie kuboresha
barabara zinazotumiwa na wakazi wa eneo hilo ili kuondoa changamoto ya
usafiri kwa wagonjwa wanaokuja kuhudumiwa.
Kampuni
ya Pan African Energy Ltd kwa mwaka 2015 inatarajia kutumia takribani
shilingi bilioni 550 kwa ajili ya kusaidia maendeleo na misaada ya
huduma za kijamii katika maeneo ambayo wanaendesha shughuli zao.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni