.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 10 Juni 2015

WAZIRI MKUU ASISITIZA UJENZI WA MAABARA ZA SEKONDARI MWISHO JUNI 30

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesisitiza kuwa tarehe ya mwisho (deadline) iliyotolewa na Serikali ya kusimamia ujenzi wa maabara za shule za sekondari iko palepale na akawataka watendaji wa Halmashauri na Mikoa kuhakikisha wanatimiza agizo hilo. 

Ametoa wito huo leo mchana (Jumatano, Juni 10, 2015) wakati akizungumza na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Waratibu wa Elimu wa Wilaya na Mikoa waliohudhuria ufunguzi wa mashindano ya UMISSETA NA UMITASHUMTA kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mashindano hayo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, alisema Serikali bado haijalegeza msimamo wake. “Tarehe 30 Juni 2015 bado iko palepale… Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya simamieni shughuli za ujenzi ili zikamilike kwa wakati,” alisema.

Alisema mbali na maabara, Serikali bado inakabiliwa na changamoto ya kumaliza tatizo la uhaba wa madawati. Alizitaka Halmashauri ziendelee kutenga fedha kila mwaka pamoja na kushirikiana na taasisi zinazosaidia jitihada za Serikali kupunguza tatizo hilo ili kuhakikisha tatizo hilo linakwisha nchini.

Waziri Mkuu pia alitumia fursa hiyo kuzungumzia tatizo la mipaka ya shule na utunzaji wa mazingira ya shule na kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya wasimamie suala hilo na kuhakikisha maeneo hayo yanapimwa na kupatiwa hati. 


“Simamieni maeneo yote ya shule yapimwe na yawe na hati miliki. Lakini wakati wa ujenzi wa shule zetu hakikisheni ramani za shule zinazingatia kuwepo kwa viwanja vya michezo ili wanafunzi waweze kufanya mazoezi na kucheza.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa vitabu, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kila mwanafunzi awe na kitabu kimoja kwa kila somo ifikapo mwaka 2016. “Hata hivyo, hivi sasa katika shule za msingi uwiano umefikia kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu (1:3) ikilinganishwa na kitabu kimoja kwa wanafunzi saba (1:7) ilivyokuwa mwaka 2005,” alisema.

Akizungumza na washiriki wa mashindano hayo kutoka kanda 12 za Tanzania Bara na Zanzibar, Waziri Mkuu aliwataka watambue kwamba michezo siyo mahali pa ugomvi bali michezo inataka nidhamu na uadilifu. “Mashindano siyo ugomvi bali ni fursa ya kujenga mshikamano, tumieni fursa hii kujenga dhamira ya kweli ya kutaka kufanya vizuri zaidi katika michuano ijayo,” alisisitiza.

Alisema washiriki wa mashindano hayo wamekutanishwa kutoka mikoa mbalimbali, na kwamba watapimwa siyo tu katika michezo, bali katika masuala mengine ikiwemo uadilifu, usafi, kuzingatia maelekezo na nidhamu. “Baadhi ya wanamichezo wana mahitaji maalum, hivyo tuoneshe upendo kwao ili wajisikie nao kushiriki katika mashindano haya,” alisisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki michezo hiyo, Waziri wa Nchi (OWM – TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia alisema mashindano hayo ni ya tano kufanyika kitaifa tangu yalipofufuliwa mwaka 2000.

Akitoa mchanganuo wa mashindano hayo, Waziri Ghasia alisema mashindano hayo yanayofanyikia Butimba, wilayani Nyamagana yataendeshwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itahusisha mashindano ya UMISSETA yaliyoanza Juni 8, 2015 na yanatarajiwa kumalizika Juni 20, mwaka huu.

“Awamu ya pili itakuwa ni ya mashindano ya UMITASHUMTA ambayo inatarajiwa kuanza Juni 22, 2015 na kukamilika ifikapo Julai 4, 2015. UMISSETA inajumuisha washiriki 1,755 wakati UMITASHUMTA itashirikisha wanamichezo 1,000,” alisema Waziri Ghasia.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni