Kikosi cha timu ya Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kinaendelea na mazoezi katika uwanja wa Amani na uwanja wa Mafunzo vilivyopo kisiwani Zanzibar.
Twiga Stars iko kambini kisiwani Zanzibar kujiandaa na fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofanyika nchini Congo- Brazzavile kuanzia Septemba 04 – 19 mwaka huu.
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage ameendelea kukinoa kikosi chake cha wachezaji 25 waliopo kambini kisiwani Zanzibar kujiandaa na michuano hiyo ya Afrika.
Twiga Stars itakua kambini kisiwani Zanzibar kwa kipindi cha mwezi mmoja, kujiandaa na fainali hizo za michezo ya afrika, ambapo imepangwa kundi A pamoja na wenyeji Congo – Brazzavile, Ivory Coast na Nigeria.
KIHANGA MWENYEKITI FA MOROGORO
Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Morogoro (MRFA) jana kilifanya uchaguzi wa viongozi wake katika nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu, mweka hazina, mjumbe wa mkutano mkuu pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Katika uchaguzi huo Paschal Kihanga aliibuka na ushindi katika nafasi ya mwenyekiti, huku Gracian Max Makota akishinda nafasi ya makamu mwneyekiti, nafasi ya katibu mkuu imechukuliwa na Charles Mwakambaya na katibu msaidizi Jimmy Lengme.
Nafasi ya Mweka Hazina imechukuliwa na Peter Mshigati, Mjumbe wa mkutano mkuu ni Hassan Mamba na mwakilishi wa vilabu ni Ramadhani Wagala, Kamati ya utendaji wamechaguliwa Mrisho Javu, Rajabu Kiwanga na Boniface Kiwale.
TFF inawapongeza viongozi wapya waliochaguliwa kuongoza chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kazi za kila siku za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
TFF YATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI MALAWI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi ametuma salam za rambi rambi kwa Rais wa Chama cha Soka nchini Malawi (FAM), Walter Nyamilandu kufutia kifo cha aliyekua Rais wa chama hicho John Zingale.
John Zangale alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi wiki iliyopita katika hospitali ya Mlambe iliyopo Blantyre nchini Malawi na kuzikwa mwishoni mwa wiki alikuwa Rais wa FAM mwaka 1998- 2002.
Katika salam zake kwenda kwa Rais wa FAM, Malinzi amewapa pole familia ya marehemu pamoja na chama cha soka nchini Malawi kwa msiba huo, na kusema TFF kwa niaba ya Watanzania iko pamoja nao katika kipindi hicho cha maombelzo.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni