Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi
ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia watoto
wanaovyojihusisha na kazi ya uvunjaji wa kokoto katika Wilaya ya
Micheweni, alipotembelea kikundi kinachojihusisha na kazi hiyo.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi
ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia kazi ya useremala
inayofanywa na wananchi wa kijiji cha Wingwi na maeneo mengine ya
Wilaya ya Micheweni.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi
ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipandisha bendera ya chama
hicho katika tawi jipya la CUF katika kijiji cha Kwale Micheweni,
kuashiria ufunguzi rasmi wa tawi hilo. (Picha na Salmin Said, OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameelezea kusikitishwa na ajira za
watoto zinazoendelea katika Wilaya ya Micheweni.
Amesema ajira hizo hazifai na
zinapaswa kupigwa vita kwa kulinda afya na ustawi wa watoto nchini.
Maalim Seif ameeleza hayo wakati wa
ziara yake ya kutembelea vikundi vya ujasiriamali katika Wilaya ya
Micheweni ambapo amejionea shughuli mbali mbali zinazofanywa na
wananchi wa Wilaya hiyo zikiwemo useremala, uvuvi, uchuuzi na
uvunjaji wa kokoto.
Amesema watoto wengi katika wilaya
hiyo wamekuwa wakijihusisha na uvunjaji wa kokoto pamoja na uvuvi na
uparaji wa samaki, mambo ambayo yanakwenda kinyume na mikataba ya
kimataifa.
Maalim Seif ambaye pia ni mgombea
urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi CUF, amesema watoto
wengi wanalazimika kujiingiza katika ajira hizo kutokana na uwezo
mdogo wa wazazi wao, na kwamba iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa
Zanzibar atabadilisha maisha ya wananchi hao kwa kuweka mazingira ya
kupata ajira zinazokubalika na zenye heshima.
Amesema serikali atakayoiongoza
itaanzisha benki ya wajasiriamali, ili kutoa mikopo kwa wananchi
kuweza kuongeza mitaji yao na kuendeleza vipaji vya wajasiriamali.
Amewashauri wajasiriamali
wanaojihusisha na kazi ya useremala kuungana na kuunganisha nguvu zao
ili waweze kuzifuata au kuagizia malighafi katika mikoa ya Tanzania
bara, ili kuepusha ukataji miti ovyo katika visiwa vya Zanzibar,
ambavyo vinakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi
yanayotokana na uchaguzi wa mazingira.
Katika risala ya wavunja kokoto
iliyosomwa na ndugu Abdalla Omar Ali, wameomba kupatiwa mitaji na
vitendea kazi vya kisasa ili kuondokana na usumbufu unaowakabili.
Nao wajasiriamali wa useremala
wamesema wanakabiliwa na upungufu wa utaalamu, zana duni za kufanyia
kazi, uchache wa malighafi pamoja na soko la kuuzia bidhaa zao, na
kuomba kutafutiwa ufumbuzi wa matatizo hayo.
Hata hivo wamesema wamenufaika na
kazi wanazozifanya ambazo zimeweza kuajiri zaidi ya watu mia tatu na
kufanya zaidi ya watu elfu tatu kunufaika na ajira hizo.
Wakati huo Maalim Seif ambaye pia
Katibu Mkuu wa CUF na mgombea urais wa Zanzibar, amefungua tawi la
CUF katika kijiji cha Kwale Micheweni, na kuwataka wananchi kuacha
kulumbana na tofauti za kisiasa.
Amesema Wazanzibari wanapaswa
kuungana kutokana na Uzanzibari wao, na kuachana kulumbana kwa mambo
ambayo hayatowaletea tija isipokuwa kuvuruga umoja na maridhiano
ambayo yaliasisiwa kwa nia njema.


Hakuna maoni :
Chapisha Maoni