.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 20 Oktoba 2015

MAALIM SEIF AUNGURUMA KATIKA VIWANJA VYA TIBIRINZI, CHAKE CHAKE PEMBA

Sehemu ya wapenzi na wafuasi wa CUF waliohudhuria mkutano kufunga kampeni katika viwanja vya Tibirinzi Pemba leo hii
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha wananchi CUF Mhe: Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wanachama na wafuasi wa CUF katika mkutano wa kufunga kampeni kisiwani Pemba uliofanyika viwanja vya Tibirinzi leo hii.
Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Maji Mkongwe, Mhe Sanya akiwanasihi wafuasi wa CUF kuwapigia kura viongozi wao katika mkutano kufunga kampeni katika viwanja vya Tibirinzi Pemba leo hii

Watoa huduma ya kwanza wakimbeba mmoja wa waliohudhuria Mkutano wa CUF baada ya kuzimia
Mgombea Uwakilishi wa jimbo la Malindi, Mhe Ismail Jussa akimwaga sera na kuwanasihi wafuasi wa CUF kuwapigia kura viongozi wao katika mkutano kufunga kampeni katika viwanja vya Tibirinzi Pemba leo hii.

                                                                                           Na Hassan Hamad (OMKR).

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha wananchi CUF Mhe: Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuwa pindi akipata ridhaa ya kuwa rais wa zanizbar, atahakikisha serikali yake inawajali na kuyathamini makundi maalumu yote.

Alisema makundi hayo ni miongoni mwa makundi muhimu katika nchi yoyote ile,katika Serikali yake atakayoiunda itayapa nafasi ya kuingia katika nafasi za maamuzi.

Maalim Seif aliyaeleza hayo huko katika viwanja vya Tibirinzi Chake Chake Pemba wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa Cuf, katika mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za Chama hicho kisiwani humo

Akizungumzia makundi hayo alisema Wanawake ni watu muhimu sana katika nchi, hivyo serikali yake haitokubali kuona wanawake wanadhalilishwa pamoja na kufanyiwa ukatili wa kijinsia hivyo itakomesha matendo hayo kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaobainika kufanya hivyo.

Kwa upande wa Vijana alisema Serikali yake itahakikisha inawathamini na kuwaheshimu pamoja na kuwapa nafasi ya kuingia katika ngazi za maamuzi, pamoja na kuwathamini watoto ambao ni mbegu ya rasilimali ya taifa.

“Ili kuweza kuishi bila ya Ubaguzi, chuki, kuthaminiwa na wajihisi wao ni moja ya sehemu ya jamii, lazima wanawake, vijana na watoto tuwape nafasi tena za juu sana ili watoto waweze kusoma na kuishi kwa raha zaidi”alisema.

Aidha Maalim Seif alisema Serikali yake itahakikisha inawaangalia walimu wanaosomesha Vyuo vya Kuran, ili kuweza kutoa taaluma ya dini vizuri.

Akizungumzia kundi la watu wenye ulemavu, alisema atahakikisha wanapatia elimu zote kama ilivyo watu wengine, ikiwemo kuwapa kipaumbele zaidi katika masuala ya ajira.

Hata hivyo mgombea huyo alisema mikakati kwenye suala la elimu, alisema ni kujenga skuli za kisasa kwa wingi kila sehemu pamoja na nyumba za walimu ili wanafunzi waweze kupatiwa elimu bila ya matatizo.

“Sisi lengo letu ni kuhakikisha watoto wanasoma na elimu inakuwa bure, kama malengo ya Marehemu Mzee Abeid Karume, mwanafunzi wa darasa lakwanza hadi chuo kikuu, pamoja na kuondosha ada za malipo kwa wananchi wote katika vituo vya afya”alisema.

Alisema serikali yake itaheshimu Umoja wa kitaifa Uliopo Zanzibar, ambao umeridhiwa na wananchi tokea 2009 kwa kupiga kura ya maoni.

Hata hivyo alilishukuru jeshi la Pilisi Zanzibar kwa kusimamia kampezi vizuri, bila ya kujali chama gani na hadi kuelekea Uchaguzi mkuu mwaka huu, kuendelea kusimamia amani na utulivu wa nchi.

Amesema wakati chama hicho kinajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu jumapili ijayo, hakuna mwanachama atakayeruhusiwa kuvaa sare za chama hicho, na kulitaka jeshi la polisi kumkamata mtu yoyote atakayeonekana amevaa sare za CUF.

Kwa upande wake Ibrahim Sanya aliwataka akinamama, vijana kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura siku itakapofika, bila ya kufanya vurugu za aina yoyote ile.

Naye Janet Fusi, aliwataka wanachama wa CUF kujitokeza kwa wingi kupiga kura, bila ya kuvaa nguo za aina yoyote ya Mgombea wala ya Chama cha siasa.

Mratibu wa kampeni za CUF Pemba Bw. Hamad MAssoud Hamad, amesema chama hicho kimefanikiwa kufanya mikutano 10 ya hadhara kwa majimbo yote 18 ya Pemba, na kwamba sasa wananchi wako tayari kwa uchaguzi.

Amesema katika mikutano hiyo CUF kilivuna jumla ya wanachama 569 kutoka Chama Cha Mapinduzi ambao walijitokeza hadharani, na wengine hadhaa ambao hawakupenda kutangazwa kwenye majukwaa ya kisiasa.

Mkutano huo wa ufungaji wa Kampeni za CUF kisiwani Pemba ukihudhuriwa na maelfu ya wanachama, umefanyika kwa mtindo wa aina yake, baada ya kutokuwepo kwa burdani ya aina yoyote mbele ya mgeni rasmi, zaidi ya kusomwa utenzi.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni