Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya
Ngorongoro, Iddi Mashaka, ambaye pia ni afisa intelijensia wa hifadhi
hiyo, amekamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio
la utunguaji wa helkopta namba 88HF na kusababisha kifo cha rubani
wake, Rogers Gower, raia wa Uingereza.
Imeelezwa mashaka amekuwa kinara
mkubwa wa ujangili katika hifadhi mbalimbali zilizopo kanda ya ziwa
kwa kutoa ushirikiano kwa majangili wenzake pamoja na kuwaazimisha
silaha za kufanyia ujangili.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo, kamanda wa polisi mkoani Simiyu, Lazaro Mambosasa, amesema
mtuhumiwa huyo ni mwajiriwa wa hifadhi hiyo ya Ngorongoro.
Kamanda Mambosasa amesema jitihada
zilizofanywa na jeshi la polisi mkoani Simiyu, zikiongozwa na mkuu wa
upelelezi, Jonathan Shana, zimeendesha msako maalum uliowashirikisha
askari wa vyeo mbalimbali, kikosi kazi na askari wanyamapori pamoja
na wananchi, wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wenzake nane
walioshiriki katika tukio hilo.
Kamanda amewataja watuhumiwa hao ni
Shija Mjika, Njile Gonga, Masasi Mandago, Mwigulu Kanga, Mapolu
Njile, Dotto Huya, Mange Balum na Dotto Pangali ambao wamedaiwa
kuhusika na tukio hilo la kikatili lililokatisha maisha ya rubani wa
helikopta iliyokuwa ikifanya doria eneo la Gululu ndani ya hifadhi ya
Maswa katika kitalu cha mwekezaji Mwiba holding ltd.
Vile vile amemtaja Dotto Pangali
ndiye aliyefanikiwa kutungua ndege hiyo kwa kutumia bunduki aina ya
rifle namba 7209460 CAR na 63229, alipohojiwa alikiri bunduki hiyo ni
mali ya Mange Magima.
Hata hivyo, kamanda Mambosasa
amesema katika tukio hilo, Shija, Njile na Masasi Mandago waliweza
kuonyesha ushirikiano wa karibu kwa kuwaonyesha meno mawili ya tembo
yenye uzito wa kilo 31 waliyokuwa wameyaficha chini ya daraja kijiji
cha Itaba.
Ameongeza mbali na tukio hilo la
kukamatwa watuhumiwa hao, meno mawili ya tembo, jeshi la polisi
waliweza kukamata bunduki 29 na risasi 141 ambazo wamiliki wake
wamekamatwa kwa ajili ya mahojiano kutokana na kukiuka masharti ya
umiliki wa silaha hizo.
Mwisho

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni