WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mabadiliko ya kiuchumi yaliyofanyika nchini yameifanya Tanzania ipige hatua kubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
"Kumekuwa na mabadiliko chanya kwenye ukuaji halisi wa Pato la Taifa, kushuka kwa mfumuko wa bei, na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni. Pato la Taifa limekua kwa wastani wa asilimia 7 na mfumuko wa bei umeshuka hadi kufikia asilimia 5.3 mnamo Juni 2015 ikilinganishwa na asilimia 16 na asilimia 8 ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka 2012 na mwanzoni wa mwaka 2013," alisema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumatano, Machi 9, 2016) wakati akihutubia kongamano la biashara baina ya Tanzania na Vietnam lililofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Bw. Troung Tan Sang.
Akizungumza kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema mbali ya mabadiliko ya kiuchumi, Tanzania pia imefanya mabadiliko kwenye sheria, mifumo ya kifedha na sekta za kuhudumia jamii za umma.
"Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita tumefanya mabadiliko ya kisera na kwenye sheria zetu ili kuboresha hali ya uwekezaji, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi," alisema.
Alitoa mwaliko kwa wafanyabiashara walioambatana na Rais wa nchi hiyo kwa kuwaeleza kwamba faida kubwa ya kuwekeza nchini Tanzania ni uwepo wa soko la uhakika kwa wakazi zaidi ya milioni 300 waishio Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika.
"Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya za Kikanda katika SADC na EAC. Uwepo wake katika taasisi hizi ni fursa tosha. Pia Tanzania ni lango kwa nchi sita ambazo hazipakani na bahari. Inasaidia kufanyika biashara katika nchi za Congo (DRC), Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Uganda," alisema.
Akizungumzia kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo, Waziri Mkuu aliwakaribisha wafanyabiashara hao wawekeze kwenye kilimo cha biashara na viwanda vya usindikaji ili waweze kusaidia kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
"Tuwakaribisha kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani za mazao yanayozalishwa nchini, kujenga viwanda vidogo vya kutengeneza vifungashio kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi. Pia mnaweza kuwekeza kwenye utengenezaji wa zana za kilimo ambazo ni za bei nafuu kwa wananchi wetu," alisema.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni