WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji wawekezaji kwenye mashamba makubwa ya kibiashara pamoja na viwanda vya usindikaji mazao ili iweze kuboresha uzalishaji nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Julai 10, 2016) wakati akifungua kongamano la siku moja la wafanyabiashara baina ya Tanzania na India lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua kongamano hilo lililojumuisha wafanyabiashara 50 kutoka India ambao wameambatana na Waziri Mkuu wa India, Bw. Narendra Modi, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Tanzania inayo fursa za uwekezaji kwenye sekta nyingi zikiwemo miundombinu, kilimo, utalii, viwanda na madini.
“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda lakini pia imelenga kuzalisha malighafi za viwanda ambavyo tunahimiza vijengwe. Lakini pia tumewaita waje kuwekeza kwenye sekta za uvuvi na utalii kwani nazo bado hazijaendelezwa vya kutosha,” alisema.
“Tanzania inazo kilometa 1,424 za fukwe za bahari, pia ina kilometa za mraba 223,000 za eneo la kiuchumi la bahari kuu (EEZ) na kilometa za mraba 54,337 za mito, mabwawa na maziwa ambayo ni sawa na asilimia 6.1 ya eneo la nchi nzima. Kuna fursa nyingi kwenye uvuvi, usindikaji wa samaki na ufugaji wa samaki kwenye mabwawa,” amesema.
Amesema washiriki pia wamepata nafasi ya kusikia fursa za uwekezaji zilizoko upande wa Zanzibar na kwamba kupitia vituo vya uwekezaji TIC na ZIPA wanaweza kupata huduma zote palepale bila kuhangaika kwenye ofisi mbalimbali.
Mapema, akihutubia washiriki wa mkutano huo, Waziri Mkuu amesema kuna fursa nyingine nyingi za kuwekeza kwenye sekta ya mifugo hasa katika uanzishaji wa ranchi za mifugo, usindikaji wa maziwa na nyama, usindikaji wa ngozi na utengenezaji wa bidhaa za ngozi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema urari wa kibiashara baina ya Tanzania na India umeegemea upande mmoja ambapo India inauza zaidi bidhaa zake hapa nchini Tanzania inavyouza bidhaa zake India. “Ninaamini njia mojawapo ya kurekebisha hali hii ni kwa wafanyabiashara kutoka India kuamua kuwekeza kwa kiwango kikubwa hapa nchini,” aliongeza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Charles Mwijage alisema Tanzania inahitaji India kama ambavyo India inahitaji Tanzania katika kufanya biashara zake. “India inaongoza kwa kuuza bidhaa zake hapa nchini lakini pia ni miongoni mwa nchi 10 ambazo zinanunua kwa wingi bidhaa zake kutoka Tanzania,” alisema.
Naye, Rais wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa India (Federation of Indian Chambers of Commerce and Industries - FICCI), Bw. Harshavardhan Neotia alisema biashara kati ya Tanzania na India inaendelea kukua na kwamba fursa zilizopo ni lazima zichangamkiwe mapema. “Fursa za kibiashara ni kama mawio ya jua, ukiendelea kusubiri sana unaweza usiyaone,” alisema.
Mkutano umejadili mada mbalimbali zikiwemo fursa za uwekezaji Tanzania bara na Zanzibar, fursa za uwekezaji kwenye maeneo ya kiuchumi, na uzoefu wa baadhi ya wafanyabiashara kutoka India walioko nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMAPILI, JULAI 10, 2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni