JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI
YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu:
255-22-2114512, 2116898
E-mail:
press@ikulu.go.tz
Tovuti :
www.ikulu.go.tz
Faksi:
255-22-2113425
|
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA
BARACK OBAMA,
11400
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ikulu,
Dar es Salaam,
Mrithi
wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais, Mtukufu Sheikh Mohamed bin
Zayed Al Nahyan amemuahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John
Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo imedhamiria kuendeleza na kukuza zaidi
uhusiano wake na Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Mtukufu
Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan ametoa ahadi hiyo kupitia kwa
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi Bw. Mohamed Al
Suwaidi aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli leo tarehe
27 Oktoba 2016.
Mfuko
wa maendeleo wa Abu Dhabi unashirikiana na Tanzania katika
utekelezaji wa miradi mbalimbali na katika mazungumzo ya leo
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo ameonesha nia ya kushirikiana zaidi na
Tanzania katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli na
barabara, usafiri wa anga na madini.
Pamoja
kumshukuru Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais Mtukufu Sheikh
Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Rais Magufuli ameialika nchi hiyo
kupitia mfuko wake wa Maendeleo na wadau wengine wa maendeleo kuja
kuwekeza hapa nchini katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa
bandari, ujenzi wa viwanda, kilimo, uvuvi, gesi na kushirikiana
katika ujenzi wa reli ya kati ambayo itazinufaisha nchi nyingine saba
za Afrika Mashariki na kati ambazo hazina bandari.
“Tanzania
imeamua kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge)
na tayari katika bajeti yetu tumetenga Shilingi Trilioni 1 kwa ajili
ya kuanza ujenzi, hivyo tunawakaribisha Mfuko wa Maendeleo wa Abu
Dhabi kushirikiana nasi, wapo wengi ambao wamejitokeza kushirikiana
nasi lakini na nyie pia tunawakaribisha, mnaweza kuchukua sehemu ya
reli na mkaijenga”
amesema Rais Magufuli.
Aidha,
Dkt. Magufuli ameutaka mfuko huo kufupisha muda unaotumika katika
mchakato wa kuanza utekelezaji wa miradi ili kuharakisha matokeo yake
na manufaa kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Oktoba, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni