Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameitumia salamu za rambirambi
familia ya Meya Mstaafu wa Jiji la Dar es Salaam Dkt. Didas Masaburi
aliyefariki dunia jana tarehe 12 Oktoba, 2016 katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Katika salamu hizo Rais Magufuli
amesema amepokea taarifa ya kifo cha Dkt. Didas Masaburi kwa mshituko
na masikitiko makubwa na kwamba anaungana na familia ya marehemu,
ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha huzuni ya
kuondokewa na mpendwa wao.
"Poleni sana familia ya Dkt.
Didas Masaburi, najua huu ni wakati mgumu sana kwenu, lakini
niwahakikishie kuwa sote tumeguswa sana na msiba huu kwa kuwa
tumempoteza mtu muhimu, msomi mzuri, kiongozi aliyelitumikia Taifa
kwa moyo wake wote na aliyesimamia kile alichokiamini" amesema
Rais Magufuli katika salamu hizo.
Aidha, Dkt. Magufuli amewapa pole
wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wamempoteza
Mwana CCM mwenzao pamoja na Viongozi na watumishi wa Jiji la Dar es
Salaam ambao walifanya nae kazi alipokuwa Meya wa Jiji.
Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu
ampumzishe mahali pema peponi.
"Bwana alitoa na Bwana ametwaa,
jina lake lihimidiwe. Amina" amemalizia Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
13 Oktoba, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni