Ni historia. Kesho ndio kesho kwa Tanzania kutengeneza historia mpya ya soka pale Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya vijana wa Tanzania ‘Serengeti Boys’ itakapoingia Uwanja wa Alphonse Massamba-Débat uliopo hapa jijini Brazzaville nchini Congo kucheza na wenyeji katika dakika 90 za mwisho za kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Katika dakika 90 za kwanza kwenye mchezo ulioofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam majuma mawili yaliyopita, Serengeti Boys ilitoka kifua mbele kwa kuwalaza vijana wa Congo kwa mabao 3-2 hivyo leo inaingia kwenye dimba la Alphonse Massamba-Débat ulioko kwenye Makutano ya Barabara za Nkolo na Boko, hapa jijini Brazzaville ikiwa na mtaji wa ushindi.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Nyundo Shime maarufu kwa jina la Mchawi Mweusi amesema kwamba amemaliza kila kitu kuhusu mchezo wa kesho ambako kwa sasa kinachoendelea ni sala na dua za kila Mtanzania kuwaombea Serengeti Boys katika mchezo huo.
Baada ya ratiba ya kifungua kinywa leo asubuhi Oktoba mosi, 2016 amewauliza nyota wake swali moja tu. “Je, mnataka nini?.. Mnataka kulia sana katika maisha yenu au mnataka kufurahi sana katika maisha yenu?”
Vijana kwa kujiamini kwa sauti ya pamoja haraka wakajibu: “Ni Faraha ya milele katika maisha yetu yote hapa duniani.” Akawaambia: “Kama ndivyo hivyo, basi tushinde…” vijana kwa marea nyingine na kwa haraka na sauti ya juu wakajibu: “Tutashinda.”
Kabla ya kuzungumza hayo leo, Shime tayari alikwisha kuzungumza akisema, “Tuko tayari kwa vita.” Katika mchezo huo unaotarajiwa kufanyika kesho Jumapili Oktoba 2, mwaka huu akisisitiza kuwa, “Timu iko vizuri. Tumejiandaa vizuri kwa yale ya msingi yote tumekamilisha. Kwa hivyo, kila kitu kiko sawa, kama tulivyokusudia.”
Shime anasema kwamba mfumo atakaoutumia ni wa 4-4-2 katika mchezo huo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana. Fainali hizo zitafanyika jijini Antananarivo, Madagascar mwezi Aprili, mwakani.
Anasema kwamba mfumo huo ni rafiki kwa Serengeti Boys kwani katika michezo takribani 15 ya kimataifa hajapoteza hata mmoja, “Kwa hivyo siwezi kubadili mfumo huu. Ni mfumo wa kushambulia na kulinda tusifungwe. Vijana wanauelewa zaidi na ndio mfumo wetu.”
Alphonse Massamba-Débat ni uwanja gani?
Uwanja wa Alphonse Massemba-Débat ambao pia unafahamika kwa jina la Uwanja wa Mapinduzi yaani Stade de la Revolution upo hapa Brazzaville. Ndio Uwanja Taifa wa Taifa wa Mpira wa Miguu katika nchi hii ya Congo. Eneo la kuchezea mpira wa miguu ‘pitch’ limezungukwa na barabara maalumu kwa ajili ya riadha na eneo la Mashariki kuna viwanja vya mpira wa mikono, wavu, netibali na mpira wa kikapu.
Uwanja huo wenye uwezo wa kubeba mashabiki 33,037 walioketi hutumiwa na klabu za CARA Brazzaville na Etoile du Congo kama uwanja wa nyumbani. Pitch yake ni ya nyasi bandia na ndio uliotumika kwa ajili ya michezo ya Afrika yaani All-Africa Games mwaka 1965 na fainali za riadha Afrika mwaka 2004.
Alphonse Massamba-Débat ni nani?
Alphonse Massamba-Débat aliyezaliwa mwaka 1921 na kufariki dunia Machi 25, 1977, alikuwa mwanasiasa mahiri katika Jamhuri ya Congo aliyeongoza nchi kuanzia 1963 mpaka 1968.
Alizaliwa Nkolo aneo ambalo linakaliwa na kabila la Lari, ambako umejengwa uwanja huo. Eneo hilo ndiko hasa Wafaransa ambako ndio walikuwa koloni la nchi hiyo. Alishiriki shule ya seminari na alipofika umri wa miaka 13 tayari alikuwa Mwalimu huko Chad.
Ilipofika mwaka 1940 akajiunga na Chama cha siasa kilichokuwa na sera za kupinga ukoloni huko Chad. Chama hicho kiliitwa Chadian Progressive Party na akafanya kazi kama Katibu Mkuu wa chama kwa ajili ya maendeleo ya chad mwaka 1945.
Mwaka 1947 alirejea Congo na kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Brazzaville ambako alijiunga na chama cha Congolese Progressive Party (PPC).
Baadaye mwaka 1957 Massamba-Débat alijiunga na chama cha Democratic Union kilichokuwa kinaongozwa na Fulbert Youlou kilichokuwa na sera ya kutetea haki za Waafrika hivyo akaachana na kufundisha kabla ya kuwa Waziri wa Elimu kabla ya baadaye kuwa kiongoza wa chama na kuwa Rais wa Congo mwaka 1963 kwa kumpindua swahiba wake, Fulbert Youlou lakini anapendwa Congo kwa sababu ya kuchechea maendelea na kupenda michezo.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni