Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekiri kuwa Wizara, Idara
na taasisi za Serikali zina matumizi madogo ya takwimu sahihi
zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini hali ambayo
inachangia kurudisha nyuma shughuli za upangaji wa maendeleo za
wananchi.
Makamu wa Rais wa Samia Suluhu
Hassan ametoa kauli hiyo leo trh 19-Nov-2016 katika hotuba yake
kwenye mahafali ya Pili ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika
(EASTC) Jijini Dar es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
ameziagiza wizara, Idara na taasisi za Serikali kuimarisha matumizi
ya takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga na kuweka mikakati ya
kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa
Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika uimarishe ushirikiano na
Wakuu wa Takwimu wa Afrika kwa kuhakikisha watakwimu wanaoingia
katika soko la ajira wanafanya kazi zao kwa kufuata misingi ya
kisheria na kanuni zake katika ukokotoaji wa takwimu zinazokubalika
kitaifa na kimataifa ambazo zitawezesha Afrika kupanga maendeleo ya
wananchi kwa ufanisi mkubwa.
Amewahimiza wahitimu wa Chuo cha
Takwimu Mashariki mwa Afrika pindi watakapoanza kufanya kazi zao
wafanye kazi kwa ufanisi na kwa umakini wa hali ya juu ili kutimiza
azma ya kutokomeza kabisa umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030
katika bara la Afrika.
“Wito wangu kwa Wizara, Idara na
Taasisi za Serikali kuhakikisha zinaimarisha vitengo vya takwimu kwa
kuwaruhusu maofisa waliopo katika vitengo vyao vya sera na mipango
wapate fursa ya kupatiwa mafunzo elekezi na ya muda mfupi kwa ajili
ya kuongeza ujuzi wao wa kuchambua na kukokotoa takwimu rasmi”
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
amesisitiza kuwa hategemei kuona wahitimu walio maliza masomo yao
katika ngazi mbalimbali katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika
wamalize soli za viatu kusaka ajira na kwamba Serikali itawawekea
mazingira bora ya kupata ajira haraka.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kushirikiana
kikamilifu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kutumia takwimu sahihi
ambazo zimetolewa na ofisi hiyo katika kupanga shughuli za maendeleo
za taifa.
Katika mahafali hiyo ya Pili ya Chuo
cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewatunuku vyeti wahitimu
133 katika ngazi za Shahada ya Uzamili ya Takwimu, Shahada ya awali
ya takiwmu na Stashahada ya takwimu kwa wahitimu kutoka nchi Kumi za
Afrika ambazo ni Nigeria,Ghana,Sierra Leon, Ethiopia,Somalia, Uganda,
Swaziland, Liberia, Rwanda na mwenyeji Tanzania.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam.
19-Nov-2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni