.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 4 Desemba 2016

WAZIRI MKUU AHOJI SABABU ZA KUTOTUMIKA KWA MBOLEA YA MINJINGU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba kufanya uchunguzi kwa nini mbolea ya minjingu inayozalishwa nchini haitumiki na badala yake inaagizwa mbolea kutoka nje ya nchi.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Desemba 3, 2016) wakati alipotembelea kiwanda cha Fibre Board 2000 Limited ambacho kinatengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo mbolea ya Minjingu, wakati akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.

Alisema mbolea hiyo licha ya kuwa na viwango vya ubora vinavyohitajika, haitumiki nchini kwa sababu ya kuingiliwa na masuala ya kisiasa dhidi ya matumizi yake.

“Nchi jirani ya Kenya inaiona mbolea hii bora kuliko sisi wa ndani? Mheshimiwa Waziri wa Kilimo are we serious? Tunazalisha mbolea hapa tunasema haina kiwango lakini Kenya wanaitaka na wameagiza tani 300,000,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa “Jambo hili lazima liangaliwe ndani ya Wizara kwa nini mnaagiza mbolea kutoka nje wakati ndani tunazalisha hii ni mianya ya rushwa, rushwa ulaji ulaji tu. Waziri lichukulie maanani jambo hili hatutaki siasa katika sekta ya kilimo,”.

Alisema kumekuwa na mijadala mingi kuhusu mbolea ya minjingu kumbe baadhi ya watendaji wanatengeneza mianya ya kwenda kununua mbolea nje ambako hutumia fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda cha Fibre Board 2000 Limited, Tosk Hansi amesema kampuni hiyo inayozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo mbolea ya minjingu, imetoa ajira kwa watu zaidi ya 1,800 wengi wao wakiwa ni vijana ila inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya urasimu wakati wanapoomba vibali vya uvunaji mazao ya misitu.

Awali, kampuni hiyo ya Fibre Board 2000 limited imemkabidhi Waziri Mkuu mchango wa madawati 1,000 kwa ajili ya shule mbalimbali za mkoani Arusha ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, DESEMBA 4, 2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni