.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 4 Januari 2017

BALOZI SEIF AZINDUA NYUMBA ZA KUISHI MAAFISA NA ASKARI WA UHAMIAJI, PEMBA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilikagua Jengo la Gorofa Mbili litakalobeba Familia Sita za Maafisa na Askari wa Uhamiaji baada ya kulizindua rasmi hapo Mtaa wa Mtukitu Chake chake Kisiwani Pemba ikiwa ni sherehe za kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi, Maafisa wa Uhamiaji na Wizara ya Mambo ya Ndani walioshuhudia ufunguzi wa Jengo la Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji chake chake Pemba. Kulia ya Balozi Seif ni Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Johari Msoud Sururu,Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Meja Gneral Projestus Rwegasira na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh., Mohamed Aboud Mohamed. Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Mwnajuma Majid,Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiam Iddi na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga.
Muonekano wa Haiba ya Jengo Jipya la Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji liliopo katika Mtaa wa Mtukitu Chake Chake Kisiwani Pemba.
Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu akitoa Taarifa ya ujenzi wa jengo la Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji wakati wa hafla ya kulizindua rasmi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Meja General Projestus Rwegasira akitoa salamu katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Makaazi ya Askari wa Uhamiaji Chake chake Pemba.
Kikundi cha Utamaduni cha Mkuta Ngoma cha Mkoa wa Kusini Pemba kikitumbuiza kwenye hafla ya ufunguzi wa Jengo la Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji Chake Chakle Pemba.


                                                                                                Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali zote Mbili Tanzania ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kujenga mazingira ya kuwapatia makaazi bora wafanyakazi wa Umma ili kuwapunguzia ukali za maisha wanayokabiliana nao kila siku.

Alisema Serikali hizo zinatambua wazi kuwa watumishi wa Umma wanapopatiwa makaazi bora ya kuishi hata utekelezaji wa majukumu yao katika maeneo ya kazi unaimarika mara dufu.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla ya ufunguzi wa Nyumba za kuishi Maafisa na Askari wa Uhamiaji hapo Mtaa wa Ndugukitu Chake Chake Kisiwani Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alisema ujenzi wa nyumba za watumishi nchini unatiliwa mkazo hasa wale wa Idara ya Uhamiaji ambao ni macho ya Taifa kwa vile muda wao wote wamekuwa wakiutumia kusimamia usalama wa Taifa kwa kuwatambua na kuwagundua wageni wote wanaoingia Nchini kinyumecha Sheria na utaratibu zilizowekwa.

Balozi Seif alisema Makubaliano ya pamoja yaliyofikiwa hapo nyuma kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu kufunguliwa kwa Ofisi ndogo za SMT Visiwani Zanzibar ni vyema yakatekelezwa haraka iwezekanavyo hasa kwa zile Taasisi za Muungano ambazo hadi wakati huu hazijaitumia fursa hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Jeshi la Uhamiaji Nchini chini ya usimamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa uamuzi wao wa busara wa kujenga nyumba za kuishi watumishi wake wakionyesha mfano mkubwa jambo ambalo ni vyema likaigwa na Taasisi nyengine za Umma Nchini.

Hata hivyo aliuomba Uongozi huo kuzifanyia matengenezo kwa wakati nyumba hizo ili kuepuka tabia iliyozoeleka ya Nyumba za Taasisi za Umma kuachwa kufanyiwa matengenezo kwa muda mrefu na kupelekea nyumba hizo kugeuka kuwa magofu.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake tayari imeshaamua kuzipatia Viwanja Taasisi zote za Muungano zinazotaka kujenga Majengo ya Ofisi pamoja na Nyumba za kuishi Watumishi wao Visiwani Zanzibar.

Balozi Seif alieleza kwamba uwepo wa Ofisi za Taasisi za Muungano Visiwani Zanzibar utaendelea kuimarisha Muungano pamoja na kuwaondoshea Wananchi wa upande wa Zanzibar wa Muungano shida ya kufuatilia huduma mbali mbali wanazozihitaji Tanzania Bara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishukuru kuona kwamba Wizara na Taasisi nyingi za Muungano tayari zimeshajenga au kufungua Ofisi zao Zanzibar akizitolea Mfano Idara ya Uhamiaji, Ofisi ya Bunge, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Benki Kuu, Costech pamoja na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Alisema Majengo ya Kisasa ya Taasisi hizo kwa sasa yamechangia katika kuvipamba Visiwa vya Zanzibar na kuipa haiba nzuri Miji ya visiwa hivi kwa majengo mazuri na ya kuvutia.

Akizungumzia hali ya Amani na Usalama iliyopo Nchini inayowapa Fursa Wananchi kufanya shughuli zao kama kawaida Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliliagiza Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji Tanzania kuendelea kusimamia vyema hali hiyo.

Balozi Seif alisema wapo baadhi ya Watu hasa wale wenye asili ya Tanzania ambao tayari wameshaukataa na kubadilisha Uraia wao wamekuwa na tabia mbovu zinazowashawishi pia kujihusisha na masuala ya Kisiasa jambo ambalo wanaelewa vyema kuwa wanavunja sheria na Taratibu za Nchi.

Aliwaonya Watu hao kuwacha tabia hizo mara moja pamoja na dharau waliyonayo ya kuwatukana Viongozi na Wananchi kitendo ambacho Serikali kamwe haitasita kuwachukulia hatua kali za Kisheria dhidi yao.

Mapema akitoa Taarifa ya ujenzi wa Nyumba hiyo ya Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji Mtukitu Chake chake Pemba Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu alisema ujenzi huo ni muendelezo wa ustawishaji wa mazingira bora ya Makaazi ya watendaji wa Jeshi hilo.

Kamishna Masururu alisema kukamilika kwa ujenzi wa Nyumba hiyo ya Ghorofa Mbili itakayobeba Familia Sita utasaidia kupunguza ifinyu wa nafasi za makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji unaolikabili Jeshi hilo katika Wilaya mbali mbali Nchini.

Alisema Jengo hilo lililoanza ujenzi wake Tarehe 5 Juni mwaka 2015 limezingatia huduma zote zinazostahiki kupatikana ikiwemo huduma za Maji, Umeme, eneo la maegesho ya Vyombo vya usafiri pamoja na huduma za watu Maalum wenye Ulemavu.

Akitoa Salamu katika hafla hiyo fupi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Tanzania Meja General Projestus Rwegasira alisema Idara ya Uhamiaji imekuwa na Mkakati wa muda mrefu katika azma yake ya kuimarisha mazingira bora ya Jeshi hillo.

Meja General Rwegasira alisema hatua hiyo imekuja kufuatia mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea Duniani likiwemo lile kubwa zaidi la Teknolojia ya Kisasa ya Habari na Mawasiliano.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mambo ya Ndani alisisitiza kwamba lengo la Idara ya Uhamiaji pamoja na masuala mengine iliyopangiwa kutekeleza, lakini pia imekusudia kujenga Ofisi sambamba na Nyumba za Kuishi Watendaji wa Jeshi hilo katika Wilaya zote Nchini Tanzania.

Jumla ya Shilingi za Kitanzania Milioni Mia 989,301,982/- zimetumika katika Ujenzi wa Jengo hilo ambapo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanbzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata wasaa wa kulikagua sehemu mbali mbali baada ya kulizindua rasmi.

Ujenzi wa Jengo la Makazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji Mtukitu Chake Chake Kisiwani Pemba uliotekelezwa na Kampuni ya Kizalendo ya Quality Building chini ya mshauri Muelekezi Mwengine Mzalendo { SAMK COSULT } ulipangwa kukamilika ndani ya kipindi cha Wiki 52.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/1/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni