Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za
Wanawake (HAWA), Joyce Kiria akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari
(hawapo pichani) mapema leo Jijini Dar, kuhusiana na uzinduzi wa
Kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wasichana na
wanafunzi wa shule za sekondari nchini Tanzania, kulia kwake Afisa
Masoko wa EATV, Brendansia Kileo.
Kituo
namba moja kwa vijana nchini cha East Africa Television LTD (EATV)
kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA) kimeanzisha
kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya wasichana wanafunzi wa
Shule za Sekondari nchini Tanzania kwa ajili ya kununulia taulo za
hedhi (Pedi) ili kuwastiri na kulinda utu wao.
Kampeni
hii inayozinduliwa leo inafanyika wakati huu ambao tukielekea Siku ya
Wanawake Duniani Machi 8, nasi kama kituo cha habari kinachofanya
biashara zake nchini tumeona tunawajibu wa kutumia vituo vyetu vya
EATV na East Africa Radio kuhamasisha jamii kuwachangia watoto wetu
wa kike kutatua tatizo hili.
Kumekuwepo na tatizo la wanafunzi wa
kike kukosa kuhudhuria shule kwa kati ya siku tano hadi saba kutokana
na kukosa pedi za kujisitiri wakati wa hedhi, ambapo kwa mwaka
inakadiriwa mwanafunzi wa kike hukosa kuhudhuria shule kwa siku 60
hadi 70 kutokana na kukosa pedi tu, hali ambayo inachangia kutofanya
vizuri kimasomo.
Wengi wa wanafunzi wa kike pia
wamekuwa wakihatarisha afya zao kwa kutumia matambara kwa ajili ya
kujisitiri wakati wa hedhi, hali ambayo pia imekuwa ikiwasababishia
aibu pale vitambaa hivyo vinapovujisha damu ya hedhi na kubainika na
wanafunzi wenzake shuleni.
Katika
kampeni hii ya kumuwezesha mtoto wa kike kuhudhuria shule bila ya
kukosa kwa sababu ya hedhi, fedha zote zitakazokusanywa katika
kampeni hii zitatumika kununulia pedi na kusambazwa kwa wanafunzi wa
kike katika shule za sekondari zitakazo chaguliwa nchini Tanzania kwa
mwaka mmoja.
Ili
kuchangia kampeni hii tunatarajia kila mwananchi atakayeguswa na
tatizo hili kuchangia kiasi cha kuanzia shilingi 5,000 tu, na fedha
zitakazopatikana zitasaidia kuwawezesha watoto wakike wengi ipasavyo
nchini kupata pedi na kuhudhuria shule kwa mwaka mzima bila kuwa na
hofu wakati wa siku zake za hedhi.
Katika
kampeni hii EATV na East Africa Radio itahamasisha uchangiaji wa
fedha na Taasisi ya Haki za Wanawake, (HAWA Foundation) iliyosajiliwa
kwa mujibu wa taratibu za nchi mwaka 2011, itahusika na kupokea na
kusimamia fedha zote zitakazochangishwa na kusimamia ununuzi na
usambazaji wa pedi hizo mashuleni.
Tatizo la wanafunzi wa kike kukosa
kuhudhuria shuleni kutokana na kukosa pedi za kujisitiri ni la kwetu
sote tuungane pamoja kuwasaidia watoto wetu wa kike ili kuhudhuria
masomo bila kukosa.
Jinsi ya kuchangia unaweza kutuma
fedha hizo kupitia kwa M-PESA
Code Namba 5530307 ama kupitia akaunti ya CRDB Namba 0150258750600.
#Namthamini


Hakuna maoni :
Chapisha Maoni