Ripota wa Globu ya Jamii alipotembelea hapo katika ukumbi wa NEXT DOOR Ijumaa hakuweza kuamini macho na masikio yake kukuta ukumbi umefurika mashabiki wakipata burudani toka kwa vijana hao. Akaamua kuhoji wahusika.
“Bendi hii tulianzisha mwaka jana (2016) mwezi wa tano na wamiliki wake ni sisi wanamuziki wenyewe tukishirikiama na wenzetu kadhaa ambao tumewaajiri”, alisema mmoja wa wamiliki wa IVORY BAND, Rama Pentagone, wakati wa mapumziko mafupi. Alisema waliamua kujiita IVORY BAND sababu ya kuangalia jina fupi litalokuwa rahisi kushikika na pia hakuna asiyefahamu thamani ya "IVORY" (Pembe ya ndovu).
Pentagone, anayepiga kinanda, gitaa na kuimba alisema wamiliki wa bendi hiyo ni yeye, mwanamuziki mkongwe mwenye sauti tamu Saleh Kupaza, Omari Kisila na Amina Juma. “IVORY BAND bado hatujatoa mtindo wa kutumia kwa sababu sisi tunapiga muziki tofauti na wengie wengine, hasa ukizingatia kwamba hatupigi “Sebene”, alisema Pentagone.
Saleh Kupaza aliyekuwa pembeni akipoza koo na maji alisema hatua ya kwanza ya kuanzisha bendi na kujiajiri wao wenyewe imefanikiwa kwa asilimia 100, na kwamba sasa wako katika hatua ya pili ambayo ni kuazalisha nyimbo kibao zenye mtazamo wa kitaiafa na kimataifa.
“Malengo yetu ya mbeleni ni kuwa kundi la muziki la Kimataifa na endapo Mungu atatujalia kutimiza malengo yetu ni kufanya maonesho makubwa ndani na nje ya nchi”, alisema Kupaza.
Omari Kisila akaongezea kwamba kwa kuwa inakaribia watimize mwaka mmoja toka waanze rasmi, IVORY BAND imepanga kufanya bonge la onesho litakaloandamana na sherehe za bendi hiyo kutimiza mwaka mmoja mnamo mwezi wa Julai.
Amesema ukumbi pamoja na tarehe rasmi ya kufanyika tukio hilo vitatangazwa muda utapokaribia, na kwamba kwa sasa wako katika hatua za mwisho za kuanza kupasua anga za redio na TV kwa kutoa kibao chao cha utambulisho kiitwacho SHIKA MOYO unachokisikia hapo chini. Hicho ni moja ya vibao takriban kumi ambavyo husisimua mashabiki kila wapigapo.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni