Kikao cha kawaida cha kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) kinakutana Jumamosi Februari 17,2018 kwenye Hoteli ya Sea Scape,Mbezi Beach,Dar Es Salam.
Kikao hicho cha kawaida kinachokutana kila baada ya miezi mitatu kitakuwa na ajenda kwa mujibu wa katiba ya TFF kupitia na kutathmini utendaji wa Shirikisho.
Kikao hicho cha kamati ya Utendaji kinatanguliwa na vikao vya kamati mbalimbali za TFF ambazo zimeanza kukutana kwa wiki mbili na wiki hii vikao vya kamati hizo vinaendelea.
Wajumbe wa Kikao cha kamati ya Utendaji wanaanza kuwasili kesho Ijumaa Februari 16, 2018 na watafikia kwenye Hoteli ya Sea Scape.
RAUNDI YA 4 ASFC KUCHEZWA FEBRUARI 21-26,TFF YAFANYA UKAGUZI WA VIWANJA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF limefanya ukaguzi wa Viwanja vitakavyotumika kwenye raundi ya 4 ya Kombe la Shirikisho la Azam ASFC.
Baada ya ukaguzi huo sasa JKT Tanzania watatumia Uwanja wa Azam Complex kwa mchezo wake dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara wakati Kiluvya United watatumia Uwanja wa Mabatini Mlandizi kwa mchezo wake dhidi ya Tanzania Prisons.
Michezo hiyo imehamishwa kwasababu ya viwanja hivyo kutokidhi viwango vya kikanuni baada ya wataalamu kutoka idara ya Ufundi TFF kufanya ukaguzi.
Ifahamike kuwa kanuni ya 7(7) ya ASFC inatamka kuwa TFF ina mamlaka ya mwisho kuhamisha mchezo husika katika Uwanja mwingine au kubadilisha kituo cha mchezo kwasababu inazoona zinafaa kwa mchezo na wakati husika.
Ratiba inaonesha kuwa Februari 21 kutakuwa na mchezo utakaowakutanisha Njombe Mji vs Mbao FC utakaochezwa Uwanja wa Sabasaba Njombe,Februari 24 Singida United watakuwa Uwanja wa Namfua Singida kucheza dhidi ya Polisi Tanzania saa 10 jioni wakati KMC watacheza dhidi ya Azam FC saa 1 usiku Azam Complex,Chamazi.
Mechi nyingine zitachezwa Februari 25 wakati Buseresere watakapowakaribisha Mtibwa Sugar saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Nyamgana nao Majimaji FC ya Songea watakuwa Uwanja wa Majimaji kuwakaribisha Young Africans saa 10 jioni na saa 1 usiku Azam Complex JKT Tanzania watawakaribisha Ndanda FC kutoka Mtwara.
Februari 26 Kiluvya United watawakaribisha Tanzania Prisons kutoka Mbeya uwanja wa Mabatini saa 8 mchana na Kambarage pale Shinyanga Stand United watacheza na Dodoma FC saa 10 jioni.
KASEKE,DIHILE WAFUNGIWA ASFC
Kamati ya mashindano ya TFF iliyokutana Februari 13, 2018 pamoja na mambo mengine ilipitia taarifa za mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam kati ya Green Warriors na Singida United ambapo wachezaji Deus Kaseke wa Singida United na Shaban Dihile wa Green Warriors wamefungiwa mechi tatu (3) na faini ya shilingi laki tano(500,000) kila mmoja kwa kosa la kutoingia uwanjani na timu zao na hawakuwepo wakati timu hizo zikipeana mikono kwenye mchezo uliozikutanisha timu hizo Januari 31,2018 mchezo namba 73 uliochezwa Azam Complex Chamazi.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya ASFC(1) ambayo inaelekeza kutumika kanuni ya ligi husika na hivyo kanuni iliyotumika ni 37(7d).
Mchezaji wa Singida United Kambale Salita amepelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya TFF kwa kosa la kumpiga mchezaji wa timu pinzani kwenye mchezo huo.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni