Hatua ya mzunguko wa Nne(4) wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam inatarajia kuanza kesho Jumatano Februari 21, 2018.
Kwenye Uwanja wa Sabasaba Njombe kutakuwa na mchezo mmoja utakaowakutanisha mwenyeji Njombe Mji atakayecheza dhidi ya Mbao FC kutoka Mwanza saa 10 jioni.
Mechi nyingine za Kombe la Shirikisho la Azam zitaendelea Jumamosi Februari 24,wakati Singida United watakapowakaribisha Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Namfua saa 10 jioni na KMC watawaalika Azam FC saa 1 usiku Azam Complex.
Jumapili Februari 25, 2018 Buseresere watakuwa uwanja wa Nyamagana Mwanza saa 8 mchana kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro,Majimaji FC ya Ruvuma watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Majimaji kuwakaribisha Young Africans ya Dar es Salaam saa 10 jioni wakati Ndanda FC watakuwa ugenini kucheza na JKT Tanzania saa 1 usiku Azam Complex Chamazi.
Jumatatu Februari 26, 2018 kutachezwa mechi mbili Kiluvya United dhidi ya Tanzania Prisons saa 8 mchana Uwanja wa Mabatini na Stand United watawaalika Dodoma FC saa 10 jioni uwanja wa Kambarage.
NDANDA VS YANGA SASA KUCHEZWA MWISHO WA MWEZI
Mchezo namba 152 wa mzunguko wa 19 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Ndanda FC ya Mtwara na Young Africans umepangiwa tarehe ya kuchezwa.
Bodi ya Ligi imetaja tarehe hiyo baada ya awali mchezo tajwa kutokuwa umepangiwa tarehe kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu.
Mchezo huo sasa utachezwa Jumatano Februari 28, 2018 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona uliopo mkoani Mtwara.
Timu zote tayari zimejulishwa kuhusu tarehe ya kuchezwa mchezo huo.
FIFA WAONGEZA TIKETI ZA KOMBE LA DUNIA KWA TANZANIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA limeongeza tiketi kwa Tanzania kwaajili ya fainali za kombe la Dunia zitakazochezwa Russia mwaka huu.
Kwa shabiki yeyote anayetaka kwenda kushuhudia fainali hizo za Kombe la Dunia awasiliane na idara ya mashindano ya TFF kwa utaratibu wa namna ya kupata tiketi hizo.
Ngwe hii ya pili ya tiketi za Kombe la Dunia imefunguliwa Februari 15, 2018 na itafungwa Machi 12, 2018.
Ikumbukwe awali FIFA walitoa tiketi 290 kwa Tanzania ili kushuhudia fainali hizo za Kombe la Dunia kabla ya zoezi hilo kufungwa mwezi Januari na sasa imefunguliwa ngwe nyingine ya tiketi hizo.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni